Loading...

NJIA 7 ZA KUBANA MATUMIZI BILA KUHISI UNAJITESA ILI KUBORESHA BAJETI YAKO

Loading...
Kama umewahi kuwa shuleni, chuoni au katika mkusanyiko wowote ule wa watu ambapo muda wa mapumziko kila mtu anajinunulia kitu anachokipenda kwa ajili ya kunywa na kula utaelewa ni nini ninachotaka kumaanisha hapa. Wengine watanunua chipsi kuku, mayai na juisi, wengine sambusa nyama na soda, wengnine supu ya mbuzi, ndizi, pilau, biriani nk. wakati wewe unajichukulia mihogo yako ya kuchemsha au ya kukaanga na maji ya bomba maarufu kama kandoro kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam lengo likiwa ni kubana matumizi ili bajeti yako isiende vibaya.

Kubana matumizi siyo kitu kibaya hata kidogo ilimradi tu kile unachotumia kina kidhi mahitaji yako na kukufanya uendelee kuishi kama ni chakula unashiba sawasawa tu na yule aliyekula biriani na kama ni kiu pia inakatika sawasawa tu na yule aliyekunywa juisi au soda. Shida haipo kwenye kukidhi haja bali ipo kwenye hisia za mtu, ile hali ya kuhisi akilini kwamba unajitesa.  Isingelikuwa hivyo wala kusingelikuwa na shida yeyote ile kwenye kubana matumizi.

Kwa bahati mbaya sana linapokuja suala la matumizi ya pesa, suala la kubana matumizi siyo rahisirahisi kama mtu unavyoweza kufikiria, hakuna mtu hata mmoja anayefurahia kujinyima kitu wakati anakiona na anaona wenzake wanatumia wala hakuna mtu anayefurahia kula ugali wa mchicha na dagaa wakati jirani yake kila siku anakaanga samaki na maini. Kusema ule ukweli hali hiyo mbaya ya kihisia hatimaye huwafanya watu wengi badala ya kuendelea kubana matumizi ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea kimaisha wanaamua kujiingiza kwenye matumizi mabaya zaidi kushinda hata ilivyokuwa mwanzoni.

Mtu anaamua kuvaa miwani ya mbao, kuvaa miwani ya mbao maana yake ni kujifanya kama vile tatizo halioni, ni sawa na mtu anayeamua kulewa pombe na kufanya mapenzi na mtu ambaye katika hali ya kawaida asingeliweza kabisa kufanya hivyo. Kwahiyo mtu anaamua kuingia kwenye matumizi makubwa na kuharibu kabisa bajeti yake bila kujali kitu kutokana na hisia zile za kujitesa anazozipata pindi anapokuwa akibana matumizi, hali ya kuhisi kutokuwa nacho, wengi huamua kujisemea, “niache niponde mali bwana kwani kufa kwaja”


NJIA ZENYEWE 7 ZA KUBANA MATUMIZI BILA KUJITESA NI HIZI HAPA;-

1. Pitia upya gharama zao zinazojirudia kila mwezi. Ili uweze kujua unatumia kiasi gani na kwa nini? kipi kimezidi na kipi cha kupunguza.

2. Kuwa mjanja kwenye manunuzi yako. Fanya tafiti za bei kabla ya kununua kitu ili upate unafuu wa gharama za manunuzi.

3. Punguza baadhi ya matumizi yasiyokuwa ya lazima.

4. Rekebisha ratiba yako ya matumizi. Badala ya kwenda sehemu za starehe kila siku kama baa na ufukweni basi tenga siku moja kwa mwezi.

5. Anzia bajeti yako sifuri. Badala ya kufanya bajeti yako kwa ule mtindo wa kujinyima na kujitesa, andaa bajeti yako kulingana tu na mapato ya mwezi husika na uridhike nayo mwenyewe bila kumlaumu yeyote wala kusononeka ukifurahia chochote ulichokuwa nacho katika hali yeyote.

6. Kuwa na moyo wa shukrani. Hapa tambua umuhimu wa kidogo ulichojaliwa sio kutaka vikubwa na wakati uwezo hauna.

7. Tengeneza pesa zaidi. Kutengeneza fedha zaidi au kuongeza kipato ni njia bora zaidi ya kumudu mahitaji yako na kupunguza hisia za kukosa zinazotokana na kubana matumizi.

Bila shaka mabadiliko haya madogomadogo kwenye bajeti yako endapo yatafanyika kwa muda mrefu matokeo yake huweza tofauti kubwa na mtu kujikuta umeboresha maisha yako pasipo kuhisi maumivu mengi.
Na Fatma Pembe.



Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com.
NJIA 7 ZA KUBANA MATUMIZI BILA KUHISI UNAJITESA ILI KUBORESHA BAJETI YAKO NJIA 7 ZA KUBANA MATUMIZI BILA KUHISI UNAJITESA ILI KUBORESHA BAJETI YAKO Reviewed by By News Reporter on 12/04/2018 08:59:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.