Serikali ya Ethiopia imetangaza hali ya tahadhari siku moja baada ya waziri mkuu kujiuzulu.
Taarifa iliotolewa na runinga ya taifa imesema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana misururu ya maandamano dhidi ya serikali ambayo yamelikumba taifa hilo.
Makumi ya watu wameuawa na wengine zaidi kujeruhiwa wakati wa maandamano hayo yalioitishwa kupigania kuwachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa.
Ni mara ya pili serikali hiyo imeweka hali ya tahadhari kukabiliana na ghasia hizo.
Kulingana na mwandishi wa habari wa BBC Emmanuel Igunza tangazo hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika ukurasa wa facebook wa chombo hicho cha taifa.
Lakini taarifa hiyo haikutoa muda utakaochukuliwa na tahadhari hiyo ama masharti ya kuwepo kwake.
Inajiri siku moja baada ya waziri mkuu Hailemariam Desalegn kutangaza kuwa anajiuzulu kutokana na mzozo ambao umekabili kipindi chake cha uongozi.
Bunge linatatarajiwa kutoka katika likizo ili kuidhinisha kujiuzulu kwake ambako tayari kumeungwa mkono na chama tawala.
Taifa la Ethiopia limekabiliwa na zaidi ya miaka mitatu ya maandamano dhidi ya serikali katika maeneo tofauti ikiwemo eneo la Oromia ambalo ndio kubwa zaidi nchini humo.
Miongoni mwa mahitaji yake ni mabadiliko ya kisiasa , haki za umiliki wa ardhi na kuachiliwa kwa wanasiasa waliofungwa.
Wiki iliopita serikali iliiwaachilia huru mamia ya wanasiasa wa upinzani na waandishi lakini maandamano yameendelea.
Mnamo mwezi Oktoba 2016, serikali ilitangaza hali ya tahadhari iliochukua miezi 10.
Hakuna maoni: