Loading...

VIONGOZI WA AFRIKA KUTIA SAINI MKATABA WA BIASHARA HURIA - KIGALI, RWANDA

Loading...
Wakuu wa nchi za umoja wa Afrika wanaokutana jijini Kigali Rwanda, Jumatano hii wanatarajiwa kutia saini mkataba wa eneo la biashara huria barani Afrika pamoja na soko la pamoja.

Wakuu hao wa nchi ambao wameanza kukutana tangu siku ya Jumatatu Machi 19, wamekutana na wadau wa sekta binafsi kuzungumzia changamoto za kibiashara zinazolikabili bara la Afrika kabla ya kutia saini mkataba huo.

Hata hivyo baadhi ya viongozi hawatahudhiria shughuli ya utiaji saini mkataba huo akiwemo rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ambaye alisema nchi yake itatia saini baada ya kukutana na wadau wengine wa biashara nchini mwake.

Rais wa Uganda pia Yoweri Kaguta Museveni amemtuma waziri wake wa mambo ya kigeni kumuwakilisha kwenye mktano huo, hatua ambayo hata hivyo imetafsiriwa tofauti na baadhi ya wadadisi wa mambo.

Hivi karibuni nchi ya Rwanda na Uganda zimeingia kwenye mzozo wa kidiplomasia huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake kwa kujaribu kuingilia masuala ya ndani na hata hivi karibuni waziri wa mambo ya kigeni wa Rwanda Louis Mushikiwabo alisema wanafanyia kazi tofauti zilizopo.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ni miongoni mwa viongozi wengine kutoka jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye hatahudhuria shughuli hiyo na kumtuma waziri wake wa mambo ya kigeni balozi Augustin Mahiga.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kuwa mkataba huu ni muhimu katika kuimarisha biashara barani Afrika hasa nchi na nchi ambapo kwa sasa mataifa ya Afrika yanafanya biashara chini ya asilimia 16.

Mkataba huu utapelekea kuazishwa pia kwa soko la pamoja ambapo nchi na nchi zitaweza kufanya biashara kwa uhuru huku wananchi wakiwa na uwezo wa kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Hata hivyo wakati viongozi hawa wakikutana jijini Kigali, kumeonekana mgawanyiko wa wazi katika nchi za Afrika kuhusu masuala ya ushirikianao na hasa kwenye biashara kutokana na ukweli kuwa sio nchi zote ambazo zitatia saini mkataba huo zikitaka muda zaidi wa majadiliano.

Kwa upande wake rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye pia ni mwenyekiti wa umoja wa Afrika amesema mkataba huu hautapunguza ufanyaji wa biashara kati ya bara la Afrika na mataifa mengine duniani kama ambavyo baadhi ya nchi zimeonesha hofu yao.

"Kuongeza biashara za ndani za Afrika haimaanishi kufanya biashara kidogo na mataifa mengine duniani. Badala yake tunapofanya biashara wenyewe itafanya makampuni yetu kukua na kuwa yenye ushindani duniani," alisema rais Kagama.

Mkataba huu wa CFTA unatarajiwa kuongeza biashara ya ndani kwa bara la Afrika kwa asilimia 52.3 kufikia mwaka 2020 na hii ni kwa mujibu wa tume ya uchumi ya umoja wa Mataifa, UNECA.

Jukumu jingine ambalo litafuata baada ya utiaji saini mkataba huu ni kwa nchi wanachama kuuridhia kwa kupitia vyombo vya maamuzi katika nchi husika.
Na Hamis Fakhi - Kigali, Rwanda.

Tuma neno 'HABARI' kwenda +255765112259 kupata habari za Afrika punde zinapojiri.
VIONGOZI WA AFRIKA KUTIA SAINI MKATABA WA BIASHARA HURIA - KIGALI, RWANDA VIONGOZI WA AFRIKA KUTIA SAINI MKATABA WA BIASHARA HURIA - KIGALI, RWANDA Reviewed by By News Reporter on 3/21/2018 09:38:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.