Loading...

UTAMU WA HALUA ZA KISIWANI PEMBA NA UNGUJA

Loading...
Kwa Zanzibar, haluwa bora kabisa inayosifika ni ya Wete ambayo ama hutayarishwa kavu ama kuwekwa lozi, ingawa kisiwani Unguja, haluwa inayopendelewa zaidi ni ya ufuta.

Haluwa huwa ina ada na kawaida zake katika jamii za Kizanzibari. Kwa mfano, adabu za kuila haluwa ni tafauti na vyakukla vyengine.

Yussuf Hemed Hamed, ambaye ni mpishi mashuhuri wa halua mjini Wete, anasema: “Haluwa hailiwi kama wali ama ugali kwa kuikamata na kuijaza kiganja tele bali huliwa kwa ncha za vidole. Tena kwa idadi maalum ya vidole, uzuri viwe viwili ama vitatu. Hapo ndipo utakapouona utamu wa haluwa.”

Haluwa nayo, huliwa ikisindikizwa na kahawa chungu na moto. Mizania hii ina maana kubwa, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, kwenye maisha ya kila siku ya watu wa Zanzibar. Ni alama ya ukweli kuhusu maisha, kwamba ni mchanganyiko wa utamu na uchungu.

Ni ishara pia ya uwiano wa siha mwilini, kwamba inapoingia sukari nyingi, basi inapaswa kuwahiwa kwa kitu kinachoiyeyusha haraka, ambacho ni kahawa. Kemikali ya Caffeine iliyomo kwenye kahawa inavunja kasi ya sukari mwilini na kuigeuza haraka kuwa maji. Ndio maana wanaokula haluwa, tende na kahawa huwa wanapata wepesi wa kupata choo cha mkojo.

Lakini maana kubwa zaidi ya mchanganyiko wa haluwa na kahawa umo kwenye mjengeko wa kijamii. Mzee Subra wa Mkungumalofa kwenye baraza ya kahawa anasema “Kahawa si kama maji au kinywaji chengine. Kahawa haifanani na kinywaji chochote duniani. Huwezi kukaa peke yako eti ukawa unakunywa kahawa. Hapo itakuwa unajidanganya tu na utakuwa unakunywa maji yako machungu. Kunywa kahawa lazima ujumuike na wenzako. Stori ziwe zimepamba moto kama ilivyo kahawa yenyewe moto, huku unapuliza taratiibu na chubuo moja moja mdomoni. Hapo ndio utakua unakunywa kahawa.”

Ladha hii ya kijamii kwenye kahawa, ndiyo iliyomo kwenye  haluwa pia. Mtu hawezi kujifungia nyumbani kwake na sahani ya haluwa mbele yake, akasema anaifaidi haluwa. Atakuwa tu anakula sukari yake. Lakini utamu wa haluwa hasa ni shughulini, kwenye harusi au Maulid, ambako sahani hupitishwa na waandaaji na kila mtu akachukua kitonge kidogo huku akizungumza na wenziwe.

Mambo haya ukiyapita bila ya kuyafikiria, utadhani hayana maana yoyote kwa Wazanzibari. Lakini ukiyafuatilia, utajua kwa nini Wazanzibari wanapenda haluwa na kahawa.
Na Fatma Pembe.




Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
UTAMU WA HALUA ZA KISIWANI PEMBA NA UNGUJA UTAMU WA HALUA ZA KISIWANI PEMBA NA UNGUJA Reviewed by By News Reporter on 5/31/2018 08:46:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.