Loading...

TAHADHARI: HALI YA UKAME NA KIPINDI KIFUPI CHA MVUA

Loading...
KITUO cha Utabiri wa Hali ya Maendeleo na Idara ya Maendeleo (IGAD) chenye makao yake makuu jijini Nairobi Kenya, kimetoa tahadhari ya uwepo wa ukame na joto kali Afrika Mashariki, huku Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), ikisema mwaka huu kutakuwa na kipindi kifupi cha mvua.

Kutokana na hali hiyo, TMA iliiwataka wananchi kujizatiti kwa kuvuna maji ya mvua na kufuata ushauri wa wataalamu kuhusu kilimo cha mazao ya muda mfupi.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri cha Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Samuel Mbuya alisema mvua hizo zitakuwa fupi za kipindi kifupi zaidi kama ilivyotabiriwa awali kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea katika ukanda wa Pembe ya Afrika na Pwani ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Katika utabiri wetu wa mwanzoni mwa Februari tuliona mvua zilitabiriwa kunyesha kwa muda mchache na kuwa kutakuwa na msimu mfupi wa Masika. Sasa hivi msimu unaelekea kuwa mfupi zaidi kwa sababu mvua zilizotarajiwa kuanza katikati ya mwezi Machi bado hazijaanza.

“Kwa hiyo mvua zitaanza mwanzoni mwa Aprili na zitakoma ndani ya wiki mbili katika baadhi ya mikoa na kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo mvua kwa sasa inanyesha inaonekana zitakoma katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili,” alisema.

Aliitaja mikoa ambayo itaathirika kwa kupata mvua chache katika kipindi kifupi zaidi ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Unguja, Pemba, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma na Morogoro.

Alisema hali hiyo inatokana na kuendelea kuwepo kwa mgandamizo mdogo wa hewa katika bahari ya Hindi, athari za kimbunga Idai kilichokumba pwani ya Msumbiji kuelekea Kusini mwa Afrika ambavyo kwa pamoja vimesababisha kutokuwepo kwa mtawanyiko wa kutosha wa mvua kama ilivyozoeleka.

Kwa upande wa taarifa ya IGAD, Tanzania, Kenya, Uganda na nchi nyingine katika Pembe ya Afrika zitaendelea kukumbwa na upungufu wa mvua wakati ukame ukitarajiwa kuongezeka kwa sababu ya hali ya ukavu inayoendelea nakuongezeka kwa joto isivyo kawaida.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa nchi hizo zitaathiriwa na ukame na joto la juu zaidi kuliko kawaida, hali itakayoathiri upatikanaji wa lishe na maji kwa watu, mifugo na wanyamapori.

“Mvua kwa kiwango cha chini Oktoba hadi Desemba mwaka jana, ikifuatiwa na joto la kawaida tangu Januari imekuwa chanzo cha kuzorota kwa kasi kwa rasilimali za wafugaji na imeanza kuathiri maisha”, ilieleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa ICPAC hali ya ukame inayochangiwa na upepo mkali wa kimbunga kwenye eneo la kitropiki la uliotokea kwenye Pwani ya Msumbiji katika wiki ya kwanza na ya pili yamwezi huu wa Machi itaendelea hadi kumalizika kwa mwezi huu wa Machi

Taarifa hiyo ilieleza kuwa maeneo yanayoathiriwa zaidi na ukosefu wa mvua ni Kusini na Mashariki mwa Ethiopia (Borana ikiwa ni pamoja na maziwa ya Bonde la Ufa na mikoa inayozunguka), maeneo ya nusu jangwa nchini Kenya na Karamoja (Uganda), Kaskazini na Mashariki mwa Somalia.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kimbunga cha kitropiki kimeiathiri Uganda kwa kuchelewesha kuanza kwa mvua hadi mwisho wa Machi. Hali ya ukame imekuwa na athari zaidi kwa kuzuia uzalishaji wa mahindi, ndizi na uzalishaji wa mimea ya wanga nchini humo.

Taarifa hiyo ya IGAD iliyotolewa kupitia kituo chake cha Utabiri na Usimamizi wa Hali ya Hewa (ICPAC) ilisema kuwa nchi maeneo ambayo yana wasiwasi juu ya usalama wa chakula ni pamoja na Karamoja nchini Uganda, Kaskazini na katikati mwa Somalia na maeneo mengi ya Sudan Kusini.

Nchini Kenya, kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ukame wa Taifa, mvua ndogo ya Oktoba hadi Desemba imeswababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wasiokuwa na uhakika wa chakula.

“Nchi zinashauriwa kuhakikisha utoaji wa maji na lishe kwa maeneo yaliyoathiriwa na ukame ili kupunguza athari za ukali wa maisha na kulinda uhai.

“Hata hivyo, kutokana na taarifa za hali ya hewa, matarajio ni kuwapo kwa siku mvua katika siku 10 za mwisho za Machi katiKa baadhi ya maeneo hivyo ni vyema kuufuatilia ufuatiliaji wa mvua ndefu katika siku kumi za mwisho za Machi, Aprili na Mei pia itakuwa muhimu kama sehemu ya kurekebisha hali mbaya iliyopo kwa sasa,” ilieleza.

ICPAC pia ilishauri mavuno ya maji kutokana na mvua inayotarajiwa inapendekezwa katika miezi miwili ijayo na mamlaka katika sekta ya afya kwa nchi zilizotajwa inapaswa kuimarisha ufuatiliaji, kufuatilia vifaa vya msingi kwa ajili ya uchunguzi na matibabu na kuboresha mfumo wa tahadhari kwa huduma za afya na za afya za mitaa.
Na Frank Malogo.




Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com.
TAHADHARI: HALI YA UKAME NA KIPINDI KIFUPI CHA MVUA TAHADHARI: HALI YA UKAME NA KIPINDI KIFUPI CHA MVUA Reviewed by By News Reporter on 3/26/2019 11:51:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.