Loading...

MJUE ALIYEVUNJA REKODI KWA KUKAA MACHO BILA KULALA KWA SIKU 11

Loading...
Binadamu kwa kawaida huwa macho mchana na usiku hulala, ingawa siku hizi si ajabu kwa wengi kulala mchana na kufanya kazi usiku.

Lakini je, umewahi kujiuliza mwanadamu anaweza kukaa muda gani bila kulala?

Vijana wawili nchini Marekani walijaribu kupima hili.

Ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka wa 1963 na bendi ya Beach Boys ilikuwa ndiyo inavuma zaidi wakati huo.

Marekani ilikuwa pia imeanza kujiingiza zaidi katika Vita vya Vietnam, na watoto wa shule za upili walikuwa wanajiandaa kwa likizo ya Krismasi pale vijana wawili walipoamua kufanya utafiti ambao ulilivutia taifa.

Utafiti huu ulifikia kikomo mnamo 8 Januari 1964.

Randy Gardner wa miaka 17 alikuwa amefanikiwa kukaa macho bila kulala kwa siku 11 na dakika 25 mfululizo.

Bruce McAllister, mmoja wa wanafunzi wa sekondari walioibuka na wazo hilo, anasema hatua hiyo ilitokana na haja ya kuunda mradi wa kuwasilisha katika maonesho ya sayansi.

Baada ya kuunganisha ubunifu wao na 'utukutu' kiasi wa ujana, Bruce na rafiki yake Randy waliamua kujaribu kuvunja rekodi ya dunia ya kukaa muda mrefu bila kulala.

Rekodi hiyo wakati huo ilikuwa inashikiliwa na DJ mmoja kutoka Honolulu, Hawaii ambaye alikuwa amekaa saa 260 bila kulala (siku 10 na saa 20).

"Mpango wa kwanza ulikuwa wa kuchunguza athari za kutolala kwenye uwezo wa kiajabu usioeleweka wa ubongo (ikiwa ni pamoja na nguvu za kiroho)," McAllister anasema.

"Tuligundua kwamba hakukuwa na njia ya kupima hilo na kwa hivyo tuliamua kupima basi athari za ukosefu wa usingizi kwenye uwezo wa mtu kufahamu na kutambua mambo, katika kucheza mpira wa kikapu. Jambo lolote tu ambalo tungeweza."

Walirusha sarafu juu kuamua ni nani angekaa bila kulala.

McAllister alifurahia sana aliposhinda kuwa 'mtazamaji'.

Lakini ulimbukeni wao ulijitokeza pale kulipozuka kikwazo cha jinsi yeye mwenyewe angemchunguza mwenzake Randy. Angefanya hivyo vipi bila yeye mwenyewe kulala?

"Tulikuwa wapumbavu. Wajua, wapumbavu wachanga," anasema "na nilikaa macho nikimfuatilia…na baada ya usiku wa tatu bila kulala, mwenyewe nilishangaa kuzinduka na kujipata nilikuwa nimelala kwa kuinamisha kichwa kwenye ukuta, na nilikuwa naandika maelezo ukutani."

Vijana hao waligundua kwamba walihitaji kumshirikisha mhusika wa tatu.

Na hapo ndipo walipomwita rafiki yao Joe Marciano kusaidia katika kuwa 'mtazamaji'.

Muda mfupi baada ya Marciano kujiunga nao, mtafiti kuhusu usingizi kutoka Chuo Kikuu cha Stanford William Dement naye alifika.

Dement kwa sasa ni profesa lakini mwaka 1964 alikuwa tu ndio anaanza kazi yake ya utafiti katika fani ya sayansi ya usingizi, ambayo ilikuwa bado changa.

Alikuwa amesoma habari kuhusu kisa cha vijana hao wawili katika gazeti moja la San Diego na akaamua mara moja kwamba alitaka kushiriki. Hilo kwa kiasi fulani liliwatuliza roho wazazi wa Randy.

"Wakati huo, pengine nilikuwa mtu pekee duniani aliyekuwa amefanya utafiti halisi kuhusu usingizi," Dement anasema.

"Wazazi wa Randy walikuwa na wasiwasi kwamba utafiti huo ungemdhuru. Kwa sababu wakati huo haikuwa imebainika kuhusu iwapo mtu angefariki kwa kukaa muda mrefu bila kulala."

Utafiti kwenye wanyama, utafiti mmoja ambao uliwashirikisha paka ambao walikufa baada ya kukaa siku 15 bila kualla, ulikuwa umeuliza maswali ya iwapo kuna mambo mengine mfano msongo wa mawazo, mfadhaiko au kemikali mwilini, ambayo huchangia kifo cha mtu aliyekosa usingizi na wala si kukosa usingizi kwenyewe.

McAllister anasema kwenye utafiti huo wa awali uliowahusisha wanyama, watafiti walitumia kemikali, jambo ambalo pengine liliathiri matokeo.

"Randy alikuwa mara kwa mara anakunywa soka aina ya Coke, lakini kando na hilo, hakunywa dawa au kemikali za kumchangamsha mtu zilizokuwa maarufu wakati huo kama vile Dexedrine au Benzedrine," anasema.

Huko San Diego kufikia wakati ambapo William Dement alikuwa anawasili, Randy, baada ya kukaa siku kadha bila usingizi, alikuwa bado mchangamfu na mwenye matumaini sana na hakuonekana akiwa na udhaifu wowote.

Lakini kadiri siku zilivyosonga, vipimo walivyomfanyia vilianza kutoa matokeo ya kushangaza.

Walipima uwezo wake wa kuonja, kunusa na kusikia na baada ya muda uwezo wake wa kutambua na kuhisi vitu ulianza kuathirika.

McAllister anakumbuka Randy akianza kusema: "Msinifanye ninuse hicho, siwezi kuvumilia harufu hiyo."

Jambo la kushangaza hata hivyo, ustadi wake wa kucheza mpira wa kikapu uliimarika.

Hili hata hivyo huenda lilichangiwa na hatua yake ya kuucheza mchezo huo zaidi.

"Alikuwa saw asana kimwili," anasema Dement.

"Kwa hivyo, tuliweza kumsaidia kuendelea kutolala kwa kucheza mpira huo wa kikapu au kucheza mchezo wa kuvingirisha matufe chini. Iwapo angefunga macho, angelala mara moja."

Usiku, ilikuwa vigumu zaidi kumzuia kulala kwani hakuwa na mengi ya kufanya, na hivyo basi wawili hao walikuwa na wakati mgumu zaidi kumzuia kulala.

Haya yote yalipokuwa yanatendeka, walianza kuangaziwa zaidi kwenye vichwa vya habari.

Wakati mmoja, taarifa yao ilikuwa ndiyo ya tatu kwa kuandikwa zaidi katika magazeti ya taifa Marekani baada ya John F Kennedy na ziara ya The Beatles.

Hata hivyo, wengi waliiangazia kama utani.

Lakini wanafunzi hao walikuwa hawafanyi mzaha na waliendelea na mpango wao bila kuvunjwa moyo.

Mwishowe, baada ya kufikisha muda wa saa 264 bila kulala, rekodi ya dunia ikawa imevunjwa na majaribio yao yakasitishwa.

Badala ya kutulia na kulala fofofo kitandani, Randy alikimbizwa hadi hospitali ya jeshi la wanamaji ambapo shughuli kwenye ubongo wake zilifuatiliwa kwa karibu.

McAllister anaeleza kilichotokea baada ya hapo.

"Hivyo analala saa 14 mfululizo - hatukushangazwa na hilo - na baadaye anaamka, zaidi ili kwenda haja. Usiku wake wa kwanza, kiwango chake cha kipindi cha usingizi uliokolea (ambao kwa kitaalamu hufahamika kama REM) ambacho wakati huo kilihusishwa na ndoto - lakini hilo lilibadilishwa baadaye - kilikuwa juu mno. Usiku uliofuata, kiwango hicho kilianza kupungua na siku chache baadaye, kiwango chake kikarejea kawaida.

"Na kisha, aliamka na kwenda shuleni…lilikuwa jambo la kufurahisha," Dement anaongeza.

Matokeo ya Randy hospitalini yalitumwa Arizona kuchunguzwa zaidi.

McAllister anasema matokeo yalionesha kwamba "ubongo wake ulikuwa unalala akiwa bado yuko macho muda wote … sehemu ya ubongo ingelala lakini nyingine ingeendelea kfuanya kazi."

Kwake, anasema, hilo linaeleweka ikizingatiwa mabadiliko ya kibiolojia yalichoangia chimbuko la binadamu wa sasa.

"Yeye hakuwa mwanadamu wa kwanza - au hata kwa viumbe waliotangulia binadamu wa sasa - kulazimika kukaa macho kwa zaidi ya usiku mmoja na kwamba kuna uwezekano ubongo wa binadamu ulibadilika ili kuuwezesha kulalisha sehemu moja nyingine ikiendelea kufanya kazi - sehemu moja ingelala na kujikarabati upya, nyingine ikiendelea kufanya kazi. Na hilo huenda lilimzuia kuathirika na ukosefu wa usingizi," anasema.

Watu wengine kadha walijaribu kuvunja rekodi ya Gardner ya kukaa muda mrefu zaidi bila kulala miaka iliyofuata.

Lakini maafisa wa Guinness Book of Records wanaotambua rekodi duniani waliacha kuidhinisha rekodi hizo, kwa sababu waliamini majaribio hayo yangedhuru afya ya wahusika.

Randy hakuonekana kuwa na dalili zozote za kuugua au kudhurika kutokana na hatua yake ya kukaa siku 11 bila kulala.

Hata hivyo, baadaye maishani alilalamika kwamba alikuwa na tatizo la kukosa usingizi.

Katika kikao na wanahabari nje ya nyumbani kwao baada ya majaribio hayo, vijana hao watatu walijibu maswali kutoka kwa umati uliokusanyika.

Randy aliwajibu kwa kutumia falsafa kuhusu majaribio yao.

"Lilikuwa tu suala la uwezo wa fikira kushinda mwili," alisema.

Tuma neno 'MAKALA' kwenda +255765112259 kupata makala za kusisimua punde zinapojiri.
MJUE ALIYEVUNJA REKODI KWA KUKAA MACHO BILA KULALA KWA SIKU 11 MJUE ALIYEVUNJA REKODI KWA KUKAA MACHO BILA KULALA KWA SIKU 11 Reviewed by By News Reporter on 2/26/2018 10:48:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.