Loading...
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imesema itazuia
uingizaji wa soseji kutoka Afrika Kusini zilizobainika kuwa na bakteria aina ya
Polony kubainika kuwa na aina hiyo ya bakteria wanaosababisha ugonjwa wa
listeriosis uliosababisha vifo vya watu 180 nchini Afrika Kusini.
Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza akizungumza na Mwananchi
jana alisema mamlaka hiyo inalifanyia kazi suala hilo ikiwa ni pamoja na kuzuia
uingizwaji wa soseji hizo nchini. “Tunalifanyia kazi kwa kufanya ukaguzi na
kujiridhisha kama soseji husika zipo katika soko,” alisema.
Soseji hizo kwa mujibu wa habari zilizochapishwa na vyombo
kadhaa vya kimataifa zinatengenezwa na kiwanda cha tiger brands unit
enterprises na cha RCL foods vyote vya Afrika Kusini. Waziri wa Afya wa Afrika
Kusini, Aaron Motsoaledi alikaririwa na mitandao ya kijamii akisema ameagiza
kuondolewa sokoni soseji hizo, huku akiwashauri wananchi kuacha kula.
Motsoaledi alisema ingawa kiwanda cha RCL hakijatajwa kama
chanzo cha ugonjwa huo, kitengo chake kinafanyiwa uchunguzi. Ugonjwa wa
listeriosis uliibuka Desemba mwaka jana na umeshasababisha vifo vya watu 180.
Akiuchambua ugonjwa huo, daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, George
Kanani alisema listeria ni aina ya bakteria ambao hupatikana kwenye maji,
udongo na kinyesi.
Alisema binadamu huambukizwa wanapotumia vyakula au maji
yenye bakteria hao. “Sababu kuu zinazosababisha listeriasis ni nyama na maziwa
mabichi,” alisema. Dk Kanani alisema bakteria hao ni hatari na husababisha kifo
wanaposhambulia mfumo wa fahamu na damu.
Alisema wanaoathiriwa kwa urahisi na bakteria hao ni watu
wenye kinga ya mwili hafifu, wenye umri wa miaka zaidi ya 65, wajawazito,
wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), wenye matatizo ya figo, kisukari na
waliofanyiwa upasuaji. Akielezea namna bakteria walivyoingia katika soseji, Dk
Kanani alisema yawezekana kulikuwa na shida katika usafi kiwandani wakati wa
kuziandaa. “Njia ya kuepuka ni usafi, kusafisha chakula, kuacha kutumia mboga
za majani mbichi, kula vyakula vilivyopikwa vizuri. Bidhaa za nyama zinatakiwa
kuandaliwa katika mazingira salama,” alisema. Tamra Capstick-Dale, mhudumu
katika duka kubwa (supamaketi) nchini Afrika Kusini la Pick n Pay alikaririwa
katika mitandao ya vyombo vya habari vya kimataifa akisema wameshaziondoa
soseji hizo katika maduka yao.
Tovuti ya kampuni ya Tiger Brands imeweka orodha ya nchi
ambazo bidhaa zake husambazwa, miongoni mwa hizo ni Tanzania.
Tuma neno 'HABARI' kwenda +255765112259 kupata habari za kitaifa punde zinapojiri.
SOSEJI KUTOKA AFRIKA KUSINI ZINAZOSABABISHA UGONJWA WA 'LISTERIA' MARUFUKU
Reviewed by By News Reporter
on
3/07/2018 10:31:00 AM
Rating:
Hakuna maoni: