Loading...

AIR TANZANIA YASHAURIWA KUJIKITA KUSHAFIRISHA WATALII KWENDA SEHEMU ZA KITALII

Loading...
CHAMA cha Mawakala wa Utalii nchini, kimelishauri Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kujikita kusafirisha watalii wanaoingia nchini kwenda maeneo ya vivutio.

Ushauri huo ulitolewa na mwenyekiti wa chama hicho,  George Chambulo,  katika kikao cha pamoja kilichowashirikisha wanachama wake, mawakala wa tiketi za ndege na maofisa waandamizi wa ATCL kutoka Dar es Salaam na Arusha.

Alisema mafanikio ya ATCL yatapatikana kupitia usafirishaji wa watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali.

Alisema, watalii wanapotua katika viwanja vya ndege vya kimataifa nchini, hawataki kusafiri kwa muda mrefu kwenda maeneo ya vivutio.

“Uongozi wa ATCL unaweza kuandaa utaratibu wa ndege zake kubeba watalii,  kwa mfano Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kuwapeleka eneo jirani la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Watalii hawataki kusafiri kwa muda mrefu, wanataka kufika mapema kwenye eneo la vivutio,” alisema na kuongeza, “wakitoka Serengeti wanataka kwenda moja kwa moja Zanzibar na kisha kurudi makwao.”

Alisema chama hicho kipo tayari kushirikiana na uongozi wa ATCL na kuwaonyesha maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa viwanja vya ndege ambayo vitakuwa maalum kwa ajili ya kusafirisha watalii.

“Unamtoaje mtalii anayetaka kwenda hifadhi ya Gombe na Katavi au Zanzibar kwa mfano, akitokea hifadhi  ya Serengeti na asichelewe ndege kurejea kwao,'' alihoji

“Tunataka kujua mpo wapi (ATCL) na kama mtanunua ndege ndogo ndogo za kutoa huduma kwa watalii itasaidia, tunajua sehemu za kujenga viwanja.

“Hatutaki viwanja vijengwe ndani ya hifadhi, la, isipokuwa vijengwe maeneo na tutawaonyesha,” alisema.

Mapema katika hotuba ya ukaribisho, Mkurugenzi Mtendaji wa ACTL, Mhandisi Ladislaus Matindi, alisema wataboresha uwezo wa ushindani katika soko.

“Tunaomba mtuelewe kwamba kuchelewa kwetu kuja kwenu, kulitokana na haja ya sisi kujipanga kwanza kabla ya kuja kwenu kama kampuni na tujiridhishe kuwa tunaweza kukidhi matakwa yenu.

“Tunaamini uwepo wa ATCL unategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano tunaouzana leo (jana). Hapa tunazungumzia kuwa karibu asilimia 80 ya wasafiri wa anga wanaokuja nchini wanategemea usafiri wa anga.

“Tumeingia makubalino na kampuni ya Hann Air ambayo itatuwezesha kuonekana katika mifumo yote ya kuuza tiketi duniani kote ndani ya kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa tumeingia mkataba na Travelport (zamani ikiitwa Gallileo),” alisema.

Alisema wapo katika mchakato kukamilisha maandalizi ya ukaguzi wa usalama (Iosa Audit) unaotarajiwa kukamilika Juni, mwaka huu.

“Tuko katika mazungumzo na IATA kuhusu kurudishiwa uanachama wetu ambao tuliupoteza miaka 10 iliyopita…hayo yote yatatuwezesha kupanua ushirikiano yetu na mashirika mengi duniani,” alisema.

Akizungumzia kupanua mtandao wa safari za nje, alisema hiyo itawezekana baada ya kuongezeka kwa idadi ya ndege kutoka nne za sasa hadi saba.

“Tunategemea kupokea bombardier CS300 mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 132 na boeing B787-800 dremliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262,” alisema.

Alisema wataalam wao walishirikishwa  katika maamuzi ya aina ya ndege za kununua, na walihusishwa katika majadiliano ya manunuzi, makubaliano ya bei, maamuzi ya namna ndege zitakavyokuwa nje na ndani kwa ndege zote.

Alisema hakuna ndege hata moja kati ya hizo wanazonunua ambayo ilikuwa tayari imekwishatengenezwa.

Na Geofrey Okechi.



Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
AIR TANZANIA YASHAURIWA KUJIKITA KUSHAFIRISHA WATALII KWENDA SEHEMU ZA KITALII AIR TANZANIA YASHAURIWA KUJIKITA KUSHAFIRISHA WATALII KWENDA SEHEMU ZA KITALII Reviewed by By News Reporter on 6/01/2018 08:11:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.