Loading...

DEFRONT UKAWA MPYA ITAKAVYOWEZA KUBAMBA SIASA KUELEKEA 2020

Loading...
Kwa mara ya nyingine Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ametambulisha wazo lake la kuanzisha muungano mpya wa ushirikiano wa vyama vya upinzani, The United Democratic Front (DeFront). Anataka DeFront iwe zaidi na mbadala ya Ukawa ya sasa.

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini alianza kulinadi wazo hili kwenye mjitandao ya kijamii mwaka jana na hivi karibuni ameutumia msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu, marehemu Kasuku Bilago, kusisitiza wazo hilo.

Bilago aliyefariki katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alizikwa nyumbani kwake wilayani Kakonko, Mkoa wa Kigoma wiki iliyopita. Katika msiba huo, ilielezwa kuwa Zitto na Mwenyekiti wa Chadema walikubaliana kushirikiana katika kuweka mgombea wa pamoja anayekubalika katika jimbo hilo bila kujali ametoka chama gani.

Wazo wa Ukawa

Kwa sasa muungano wa vyama ulipo ni Ukawa. Huu unaunganisha vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF ambayo sasa imegawanyika pande mbili. Upande wa Katibu mkuu, Seif Sharif Hamad unakubaliana na Ukawa, lakini ule wa Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba unaipinga.

Ukawa ni wazo lililoibuliwa na Profesa Lipumba wakati wa mjadala wa Katiba Mpya, ukilenga kuwaunganisha wajumbe, wakiwamo wa vyama vya upinzani waliokuwa wanataka rasimu iliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba ipitishwe.

Hata hivyo, pamoja na kushindwa, umoja huo uliendelezwa ukiwaunganisha wapinzani katika harakati za kisiasa, ingawa chama cha Zitto, ACT-Wazalendo na vingine havikujumuishwa.

Zitto ajisogeza

Akizungumzia muungano anaopigania sasa, Zitto anasema amekuwa na dhamira ya kuona vyama vya upinzani vikiunganisha nguvu dhidi ya CCM katika chaguzi mbalimbali.

Alisema kwa heshima ya mwalimu Bilago yeye na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wamekubaliana kuanzisha The United Democratic Front (ushirikiano wa kidemokrasia) kuanzia katika Jimbo la Buyungu.

“Tunataka kuweka mgombea mmoja anayekubalika na wananchi wa Buyungu na kufanya kampeni kwa pamoja mpaka ushindi,” anasema Zitto.

Mbowe atia tiki

Mbowe kwa kuonyesha kuunga mkono wazo hilo, alimsimamisha Zitto katika msiba huo na kusema kuwa wako tayari kushirikiana na vyama vingine na muungano huo utakwenda nchi nzima.
Lakini, baadaye akizungumza na Mwananchi, Mbowe alisema hawapingi ushirikiano wa vyama bali wanataka “kutafakari zaidi kuhusu vyama wanavyoungana navyo”.

Vilevile, Mbowe anasema hilo haliko katika mamlaka yake pekee, bali vikao vya chama.

“Tumezungumzia suala la kuweka mgombea mmoja atakayekuwa na nguvu ya kushinda, lakini hilo si suala la mimi kusema tu, ni la vikao vya chama.”
Na Neema Joshua.




Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
DEFRONT UKAWA MPYA ITAKAVYOWEZA KUBAMBA SIASA KUELEKEA 2020 DEFRONT UKAWA MPYA ITAKAVYOWEZA KUBAMBA SIASA KUELEKEA 2020 Reviewed by By News Reporter on 6/06/2018 08:47:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.