Loading...

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UUZWAJI WA VIFAA VYA KUJIPIMA UKIMWI MADUKANI

Loading...
Wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kubadilisha sheria ili kuruhusu watu kujipima wenyewe Virusi vya Ukimwi (VVU), imepiga marufuku uuzwaji wa vifaa vya kupimia virusi hivyo kwa watu binafsi.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amepiga marufuku uuzwaji wa vifaa hivyo kwa watu binafsi, akisema hatua hiyo inatokana na sheria za nchi kutoruhusu mtu kujipima mwenyewe.

Dk Ndugulile alisema hayo jana baada ya hafla ya kukabidhi cheti cha ubora wa kimataifa (Iso), kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF). Alisema sheria iliyopo sasa inaruhusu mtu kupimwa VVU na mtaalamu au mtoa huduma kutoka kituo cha afya na si vinginevyo.

“Hivi sasa bado tuko katika hatua ya kubadilisha sheria ili tuweze kuruhusu watu kujipima wenyewe, lakini hii itakuwa baada ya majaribio yanayofanyika katika baadhi ya maeneo kuonyesha matokeo chanya,” alisema.

Aliziagiza taasisi zinazohusika kuhakikisha zinadhibiti uuzwaji holela wa vifaa hivyo kwenye maduka ya dawa na vifaa tiba nchini.

Mei 31, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema wamemwandikia barua Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili kubadili sheria kumwezesha kila mtu kujipima VVU nyumbani.

Ummy alisema hayo bungeni akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtambulie (CUF), Masoud Abdalla Salim aliyeuliza mkakati wa ziada wa Serikali wa kutambua watu wanaopata athari za VVU.

“Nchi nyingine wanatumia mate kutambua waathirika wa VVU, Serikali ina mkakati gani wa ziada kutambua wale wanaopata athari za VVU hasa tukianza na Mkoa wa Dodoma,” aliuliza Salim.

Akijibu swali hilo, Waziri Ummy alisema sheria imekuwa kikwazo kwa wananchi kujipima maambukizi ya VVU.

Alisema kipimo hicho kinamwezesha mtu kujua hali yake ndani ya dakika 15 na hivyo kitasaidia katika mapambano dhidi ya Ukimwi. Baada ya majibu ya waziri, baadhi ya wadau walipinga mpango huo wakisema una madhara kulinganisha na faida na wengine wakisema iwapo miongozo itafuatwa, utakuwa na manufaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Leonard Maboko alisema kama utawekewa utaratibu mzuri, utaongeza ari ya watu kutambua afya zao.

Wakati huohuo, Dk Ndugulile alisema kabla ya mwaka huu kuisha, Serikali itakuwa na sheria ya bima ya afya kwa wananchi wote. Alisema sheria hiyo itamlazimisha kila mwananchi kuwa na bima ya afya kama ilivyo kwa kitambulisho cha uraia ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kuwafanya Watanzania wengi kuwa na bima hiyo.

Alisema Serikali imedhamiria kuwa ifikapo mwaka 2020 asilimia 80 ya Watanzania wawe na bima za afya, jambo ambalo litawasaidia kupunguza gharama za matibabu.

“Lakini wakati tunaelekea huko nataka NHIF mpanue wigo wa vifurushi vya huduma vitakavyowawezesha watu wengi kumudu gharama au kila mtu kujipimia aina ya kifurushi anachotaka kulingana na mahitaji, na kuwafikia watu wote hata wasioajiriwa wala kuwa katika vikundi,” alisema Dk Ndugulile.

Alisema siyo lazima kuwapo kwa kadi za aina nyingi, bali aina moja inaweza kuwekewa madaraja kulingana na aina ya huduma na gharama zake.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema wanasubiri kibali kutoka serikalini ili kuanzisha vifurushi vipya vitakavyompa kila Mtanzania fursa ya kuchagua huduma anayoweza kumudu.
Na Mary Mkeu.




Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UUZWAJI WA VIFAA VYA KUJIPIMA UKIMWI MADUKANI SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UUZWAJI WA VIFAA VYA KUJIPIMA UKIMWI MADUKANI Reviewed by By News Reporter on 8/21/2018 10:08:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.