Loading...
KATIKA jitihada za kuendelea kuitangaza Zanzibar kama kituo cha utalii Duniani, Zanzibar inatarajia kuandaa tamasha la utalii la siku tatu lenye lengo la kuimarisha sekta ya utalii na kuanisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chama miaka 20 tokea serikali ilipofungua milango ya utalii na uwekezaji nchini.
Tamasha hilo lililopangwa kufanyika Oktoba 17-20 mwaka huu katika hoteli Verde Mtoni, litabeba ujumbe usemao ‘Utalii unaozingatia mazingira, ustawi bora wa jamii.”
Makamu Mwenyekiti wa kamati inayosimamia tamasha hilo, Javed Jafferji, katika taarifa yake, alisema mipango inachukuliwa kuhakikisha tamasha hilo linafanikiwa ikiwemo kuzinduliwa kamati ya usimamizi, na ufundi na zawadi, zinazojumuisha wanachama wanane wenye ushawishi kutoka sekta ya umma na binafsi.
Alisema kamati inaundwa na watu kutoka serikalini, sekta binafsi na vyama vya kiraia ambao wana uzoefu katika masuala ya utalii.
“Zanzibar ina furaha kutangaza uzinduzi wa tamasha la utalii, tukio la pekee linaloonesha utayari wa serikali kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii. Zanzibar inaendelea vizuri katika sekta hii kwa miaka 20 iliyopita na tokea serikali ilipofanya mageuzi ya kiuchumi,” alisema Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Mahmoud Thabit Kombo.
Alisema utalii ni moja ya sekta muhimu zaidi Zanzibar inayochangia asilimia 27 ya pato la taifa. Imeajiri jumla ya watu 45,000, ambao ni zaidi ya asilimia 10 ya jumla ya idadi ya watu walioajiriwa Zanzibar. Takwimu hiyo inajumuisha wananchi wa Zanzibar na wasio Wazanzibari, ambao wameajiriwa moja kwa moja katika sekta ya utalii au kazi zenye uhusiano na utalii.
Jafferji alisema tamasha hilo lina lengo la kukuza utalii na uwekezaji na kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta hiyo.
“Licha ya kuwa na fukwe zenye mchanga mweupe, Zanzibar ina idadi nzuri ya wawekezaji hasa katika hoteli, kampuni za watembezaji watalii, safari za ndege za kimataifa – zote zina mchango mkubwa katika utalii wa Zanzibar,” alisema.
Jafferji, alisema tamasha la utalii la Zanzibar 2018 lina lengo la kukuza vyote, utalii na uwekezaji Zanzibar ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha ajenda ya maendeleo ya Zanzibar inafikiwa.
NA Fatma Pembe.
Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
ZANZIBAR YAJIPANGA KUANDAA TAMASHA LA AINA YAKE LA UTALII
Reviewed by By News Reporter
on
8/26/2018 09:44:00 AM
Rating:
![ZANZIBAR YAJIPANGA KUANDAA TAMASHA LA AINA YAKE LA UTALII](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgghbU-pi3K1LkDLD_rFMfRtFjmxOkqB6MHwsBnGmNTmcPrsWiyZ6LqrauDH5WtZOw0YAQmB5S6LeFfvHCJXXgNabMbk3y_YFXLwNyj8-pxYHEc1NzvBErct2v9h9U4faqDurIwhr8DsxQ/s72-c/ZANZIBAR+KUANDAA+TAMASHA+LA+AINA+YAKE+LA+UTALII.jpg)
Hakuna maoni: