Loading...
- Wakina baba tumeusiwa kwamba ili tujenge familia zenye upendo tunapaswa kuwajibika kikamilifu katika majukumu yetu.
- Sisi ndio wa kujenga au kubomoa familia kwa kuwa kimaadili na kitamaduni sisi ndio inaaminika ndio viongozi katika taasisi za ndoa zetu.
- Baba usipo yazingatia haya yafuatayo unaweza ukajikuta familia yako inakosa upendo, maendeleo na furaha. Mambo yenye ni kama; Usiwabague watoto, Usifanye mke na watoto wakuogope, Usiwe muamuzi pekee wa mambo yote yanayowahusu wanafamilia yako, Usiwalaumu sana wanafamilia wanapokosea na mwisho Mwanafamilia akikosea ichukulie kuwa ni fursa.
Baba ukitaka ujenge familia yenye upendo, ushirikiano na furaha kupata maendeleo epuka yafuayayo:-
1) usiwabague watoto wako kulingana na tofauti zao za kihulka na kimatashi. Tumeumbwa kuwa tofauti kwa vitu tofauti ikiwemo mitazamo. Wanaopitiliza kwa hulka mbaya warekebishwe kwa nguvu zote bila kiwatoa kundini
2) usifanye mke na watoto wakuogope. Jitahidi kufanya wawe na adabu na upendo kwako kwa kuwatendea haki na hakikisha kila mmoja nyumbani kwako anastahili heshima, hata mtoto wako wa chekechea. Uoga hupoteza hali ya mtu kujiamini, kuwa mbunifu na kuwa jasiri. Uoga unajenga chuki ya waliotishwa kwenda kwa mtishaji.
3)usiwe mwamuzi pekee wa mambo yote yanayowahusu wanafamilia wako. Wanayo mengi ya kujifunza toka kwako kama nawe ulivyo na mengi ya kujifunza toka kwao. Kubadilishana mawazo kuhusu mambo makubwa ya kifamilia ni msingi wa maendeleo.
4) wewe baba ndiye mfariji mkuu wa familia. Mkeo au mtoto akitapeliwa kizembe au akiibiwa kizembe, usimfokee na kumuonesha jinsi alivyo mjinga, mpuuzi na mshamba. Itakuwa kumuongezea maumivu juu ya maumivu. Kwa sauti ya huruma mpe pole na mfariji kwa kumtia moyo wa kupata zaidi ya alichopoteza kwani bado anao uhai. Ila msisitize awe mwangalifu kuhakikisha hapati tena hasara kwa njia hiyo au inayofanana na hiyo. Kuwa mfariji kwa shida zote za wanafamilia wote.
5) Mwanafamilia anayekosea kutenda jambo la kifamilia ni mtendaji na mbunifu. Elewa, kwanza, asiyetaka au anayeogopa kukosea huwa hafanyi jambo. Mtendaji wa ukweli lazima kuna wakati hukosea. Pili, mafanikio yote duniani tunayoyaona na kuyasikia, yamepatikana kwa kuingia kwenye 'risk'. Huwezi kufanikiwa ukitaka uwe 'completely free from risk'. Kwa hiyo usikimbilie kumuadhibu mtoto wako atakayekosea kutekeleza jukumu ulilompa. Chunguza uone kama kukosea kwake ni kwa nia njema ya kuboresha ulichomtaka afanye, au ni kwa uzembe ama kwa nia ovu (hili la mwisho halitarajiwi). Mrekebishe na mtie moyo wa kutekeleza kwa usahihi. Ukimuadhibu na kumpa jukumu hilo mtoto mwingine, ujue huyu wa pili atakuwa boya kwa kutotenda chochote kuogopa kukosea.
Usije ukashangaa familia ya wenye kipato duni na elimu ya chini ya wanafamilia inakuwa na upendo, maendeleo na furaha tofauti na ya kwako yenye kipato kikubwa na elimu za juu. Familia ile ya wanyonge imezingatia matano ya hapo juu, miongoni kwa mengine mazuri. Kazi kwetu kina baba.
Na Geofrey Okechi.
Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com.
USIA KWA WAKINA BABA WENYE MAJUKUMU
Reviewed by By News Reporter
on
10/28/2018 09:12:00 AM
Rating:
Hakuna maoni: