Loading...

ATCL KUANZA KUPAA RASMI KUELEKEA MUMBAI, INDIA JULAI 17

Loading...
SAFARI ya kwanza ndege za Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kwenda Mumbai, India itazinduliwa Julai 17, mwaka huu huku dirisha la kukata tiketi kwa safari hizo tayari limefunguliwa rasmi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema hatua hiyo ni mafanikio ya Mpango Mkakati wao ulioanza mwaka 2017, waliojiwekea kuhakikisha shirika hilo linapata mafanikio kwenye usafiri wa anga kwa kufungua vituo vingi vya biashara nje ya nchi.

Matindi alisema kwa sasa wamefungua rasmi dirisha la kukata tiketi kwa safari za Mumbai, India, ambapo wasafiri wanaweza kununua tiketi hizo kupitia mtandao wa shirika hilo, kwa mawakala wa ndege na pia wanaweza kufanya malipo kwa kutumia kadi za benki, Mpesa au Tigopesa na kulipa papo hapo wakati wa kununua tiketi dirishani.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa ATCL, Josephat Kagirwa alisema bei za kuanzia zitakuwa kati ya Dola za Marekani 286 hadi 460 kwa ruti moja, ambapo kwa fedha ya nchini safari ya kwenda na kurudi kwa daraja la kawaida itakuwa Sh milioni 1.4.

Aidha kwa daraja la juu safari ya kwenda na kurudi, itakuwa Sh milioni 4.3 na kwamba bei hiyo ni nafuu ukilinganisha na bei za kampuni nyingine za ndege kwenda safari kama hiyo. “Tumeamua kuanzia na bei hiyo ya promosheni kwa muda kama njia ya kuitangaza ndege yetu ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 282,” alisema Kagirwa.

Alisema ndege hiyo ya Dreamliner itakuwa ikifanya safari hizo mara tatu kwa wiki na kwamba maandalizi yake yamekamilika. Wakati huo huo, Matindi alizungumzia kuzinduliwa kwa safari za kwenda Afrika Kusini katika Jiji la Johannesburg na kusema Juni 28, mwaka huu, watazindua safari katika jiji hilo ambapo nauli ya kwenda na kurudi itakuwa Dola za Marekani 300 takribani Sh 700,000.

Alisema safari katika ruti hiyo itahusisha ndege mpya za Air Bus A220-300 na kwamba uzinduzi wa tiketi kwa ajili ya safari hizo, umefunguliwa rasmi na kuwataka wananchi na wasafiri kutumia fursa hiyo kupanda ndege hizo mpya.
Na Geofrey Okechi.
.
.
Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com.
ATCL KUANZA KUPAA RASMI KUELEKEA MUMBAI, INDIA JULAI 17 ATCL KUANZA KUPAA RASMI KUELEKEA MUMBAI, INDIA JULAI 17 Reviewed by By News Reporter on 5/17/2019 10:31:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.