Loading...

50% YA WAHITIMU VYUO VIKUU AFRIKA MASHARIKI HAWANA SIFA ZA KUAJIRIWA

Loading...
Chama cha Waajiri Afrika Mashariki (EAEO), kimesema nusu ya wahitimu wa vyuo vikuu katika nchi za ukanda huo hawana sifa na ujuzi wa kuajiriwa.

Wakizungumza jana katika mkutano wa nne wa mwaka wa EAEO, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Aggrey Mlimuka na mwenyekiti wake, Rosemary Ssenabulya, walisema ni muhimu tatizo la kukosa sifa za kuajiriwa kwa wahitimu hao likafanyiwa kazi na wadau wote.

Dk Mlimuka alisema utafiti ambao umefanywa unaonyesha vyuo vikuu na vya kati katika nchi zote za Afrika Mashariki, vinatoa elimu ambayo inawafanya vijana washindwe kuajiriwa.

Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, lazima vyuo viandae vyema wahitimu kwa kuwapo na uhusiano baina ya mitaala ya masomo na mahitaji katika soko la ajira.

“Nilimsikia Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa alielezea jambo hili napenda kueleza tatizo hili lipo katika nchi zote, lazima sasa mafunzo ya vyuo yajibu changamoto sehemu za kazi na kuwapa ujuzi wahitimu,” alisema Dk Mlimuka.

Alisema ni muhimu vyuo vikuu na vya kati vitoe elimu ambayo inawawezesha vijana kupata ujuzi wa kuweza kujiajiri.

“Kuna haja ya kubadilika, tusisahau ajira zitakuwapo, watu wanaweza kujiajiri, tunapaswa kujiuliza tunatoa mafunzo gani ili watu waweze kujiajiri,” alisema.

Hata hivyo, Dk Mlimuka alisema waajiri katika kukabiliana na tatizo hilo sasa wameanza kuhimiza kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa vyuo.

Naye Ssenabulya alisema tatizo la ukosefu wa ujuzi kwa wahitimu wa vyuo vikuu Afrika Mashariki, limekuwa likiwaathiri zaidi waajiri.

Alisema ndiyo sababu sasa waajiri wanatafuta wafanyakazi kutoka nje ya Afrika Mashariki, wenye uwezo kwa gharama kubwa zaidi.

“Bado tunaendelea na mikakati kuwaunganisha waajiri kupitia chama hiki, ili waweze kushiriki kwa pamoja mikakati ya kusaidia kuongeza ajira kwa wakazi wa Afrika Mashariki,” alisema.

Hata hivyo, Ssenabulya alisema waajiri wengi hawajui umuhimu wa EAEO katika kusaidia kuongeza uzalishaji wao, kukuza mitaji na kupunguza migogoro maeneo ya kazi.

Akizungumzia tatizo la ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu, katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Eric Shitinde alisema Serikali tayari imeanza kuchukua hatua na imeandaa mwongozo wa Taifa wa uanagenzi na mwongozo wa Taifa wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa vyuo ili waweze kuajirika.

Shitinde alisema tayari vijana 3,660 wameandikishwa kupata mafunzo mbalimbali ya kuwajengea ujuzi kwa njia ya uanagenzi na tayari 1,447 wamehitimu.

Alisema Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2018, inaendelea kukamilishwa na hivi karibuni itapelekwa kwenye baraza la mawaziri.

Kila mwaka, zaidi ya vijana 60,000 wanahitimu vyuo vikuu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
Na Geofrey Okechi.


Tuma neno 'HABARI' kwenda +255765112259 kupata habari za kitaifa punde zinapojiri.
50% YA WAHITIMU VYUO VIKUU AFRIKA MASHARIKI HAWANA SIFA ZA KUAJIRIWA 50% YA WAHITIMU VYUO VIKUU AFRIKA MASHARIKI HAWANA SIFA ZA KUAJIRIWA Reviewed by By News Reporter on 3/26/2018 10:17:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.