Loading...

AHADI YA SH50 MILIONI UTATA MTUPU BUNGENI, WAZIRI MPANGO ATOA UFAFANUZI

Loading...
Bunge jana lilimbana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango likitaka maelezo ya utekelezaji wa ahadi ya kutoa Sh50 milioni kwa kila kijiji, likionya kuwa suala hilo linaweza kuisumbua CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Fedha hizo zilizoahidiwa na CCM kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, Waziri Mpango alisema jana jioni kuwa zitatolewa baada ya utaratibu kukamilika.

Wakichangia katika bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2018/19, wabunge walisema imebaki miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu, lakini utekelezaji wa ahadi hiyo haujaanza.

“Ni vizuri waziri akikaa pale jioni akatuambia hizi fedha zipo au huu mpango haupo kwa sababu ni kazi kubwa mwaka 2020,” alisema mbunge wa Muheza (CCM), Balozi Adadi Rajabu.
Alisema ahadi hiyo imewaletea matatizo makubwa.

“Mwaka wa fedha 2016/17 suala hilo lilitengewa Sh60 bilioni na mwaka wa fedha 2016/17 lilitengewa tena Sh60 bilioni, lakini hadi sasa hakuna hata senti moja iliyotolewa,” alisema.

Mbunge mwingine aliyechangia suala hilo ni wa Mbeya Mjini (Chadema) Joseph Mbilinyi aliyesema wapinzani si tu wana Ilani ya uchaguzi ya CCM, bali pia orodha ya ahadi zilizotolewa wakati wa uchaguzi.

“Jiji la Mbeya lina mitaa 181 ambayo (wakazi wake) wanasubiri Sh50 milioni kila mtaa na wana kazi ya kuzifanyia,” alisema.

Wengine waliochangia ni pamoja na mbunge wa Babati Vijijini (CCM), Jitu Son, David Silinde (Momba-Chadema) na Suzani Kiwanga (Mlimba-Chadema).

Lakini wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na John Mnyika (Kibamba) waliibua upya mjadala wa Sh1.5 trilioni ambazo ni tofauti ya fedha zilizokusanywa na zikakaguliwa na zile zilizokusanywa lakini hazikukaguliwa, kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17.

Mchango wa wabunge hao uliibua mvutano kati yao na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama.

Waziri Mhagama alisimama mara kadhaa, kutoa taarifa kwamba ripoti za CAG hazijadiliwi ndani za Bunge hadi baada ya kujadiliwa na kamati husika.
Hata hivyo, wakati wote ambapo Waziri Mhagama aliposimama kutoa taraifa hiyo, wabunge wa upinzani walimpinga na baadhi walisikika wakisema “mbona nyinyi mawaziri mlizizungumzia?”.

Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga alikuwa na wakati mgumu kuongoza mjadala huo, akijaribu kuwasihi wabunge, hasa wa upinzani, watulie kumsikiliza Waziri Mhagama huku Mnyika na Mdee wakipinga wakitaka kuachwa wachangie.

Mvutano huo ulianza wakati Mnyika aliposema Wizara ya Fedha imekuwa na kawaida ya kutoa kauli zenye shaka bungeni na hazipashwi kuaminika.

“Aprili 20 mwaka huu ndani ya Bunge hili, Naibu Waziri wa Fedha (Dk Ashatu Kijaji) alitoa kauli humu bungeni akifafanua kuhusu utata wa Sh1.5 trilioni ambazo hazijulikanani zimeandea wapi,” alisema.

Katika kauli yake akalieza Bunge kwamba Sh209 bilioni ni fedha ambazo zimepelekwa Zanzibar. Nimefuatilia mjadala wa Baraza la Wawakilishi, nimepitia ripoti ya BoT, mpaka sasa hakuna anayeeleza Sh209 bilioni zilipelekwa lini, zilipelekwa katika akaunti gani na zilipekewaje.”

Kauli hiyo ilimfanya Waziri Mhagama kutoa taarifa kuwa kauli za mawaziri huwa hazijadiliwi bungeni na kusababisha kuibuka tena kwa kelele.

“Pili, utaratiubu wa shughuli ya ripoti za shughuli yoyote inayotokana na ripoti za CAG, umewekwa kwa mujibu wa kanuni. Itakuja kujadiliwa baada ya kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuijadili na kutoa taarifa,” alisema.
Alisema mawaziri waliijadili hoja ya CAG nje ya Bunge.

Hata hivyo, Mnyika alisema CAG anapaswa kuchunguza utata wa Sh1.5 trilioni na deni la taifa.

“Kimsingi (hii) ni bajeti ya kukopa na kulipa. Tunakopa Sh8 trilioni tunalipa Sh10 trilioni na fedha kwa kiwango kikubwa ni mkopo wa kibiashara, kwa hiyo uchunguzi unahitajika,” alisema.

Baadaye Mdee alisema: “Naibu Spika aliwahi kusema hapa bungeni kwamba kuzungumzia taarifa za CAG ni suala halali na kila mtu anayo haki ya kuzungumzia ripoti za CAG na wabunge tuna haki ya kujiachia katika ripoti za CAG

“Tunamtaka Waziri wa Fedha atujibu atuambie Sh1.5 trilioni atujibu zipo wapi, atuambie Sh200 bilioni mlizopeleka Zanzibar ziko wapi, zimepelekwa lini, kwa usafiri gani na zilifanya nini.”

Baada ya kauli hiyo, Waziri Mhagama alisimama tena, kutoa utaratibu huku Mdee akisema, “akae chini (Waziri Mhagama) ananipotezea mda, atasema yale yale.”

Mwenyekiti wa Bunge, Giga alimtaka Mdee kukaa chini na Waziri Mhagama akasema, “tunachotaka, hoja ya CAG majibu yake kwa mujibu wa sheria ya bajeti, sheria zote za fedha, hoja hizi ambazo Halima anazisema Serikali zitakwenda kujibiwa katika kamati husika.”

Mara baada ya kuruhusiwa kuendelea, Mdee alisema “tumekusikia (Waziri Mhagama), (Rais John) Magufuli amekusikia unavyopambana, kaa chini.”
Mdee akiendelea kuchangia alisema, “Waziri wa Fedha akija hapa atuambie zile fedha za makinikia zipo wapi.”

Alisema alisema anaona aibu kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuwa mwalimu wake kwasababu ameshindwa kulieleza bunge kuhusu Sh 424 trilioni ambazo Serikali ilidai zitalipwa na Mgodi wa Acacia kama kodi waliyokwepa.

Alisema wakati Profesa Kabudi akizungumza bungeni alisema hawatasema tena kiasi wanachodai kwa makampuni hayo kwasababu kuna watu wanaibuka kuidai nchi.

“Tuliwahi kusema kuwa shida sio Acacia, shida ni Serikali. Naona aibu kusema kuwa Kabudi ni mwalimu wangu waziri anasema kuwa hawezi kutamka kiasi gani kimelipwa kwasababu watakuja watu wanaotudai,” alisema
Na Geofrey Okechi.




Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
AHADI YA SH50 MILIONI UTATA MTUPU BUNGENI, WAZIRI MPANGO ATOA UFAFANUZI AHADI YA SH50 MILIONI UTATA MTUPU BUNGENI, WAZIRI MPANGO ATOA UFAFANUZI Reviewed by By News Reporter on 6/07/2018 10:34:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.