Loading...

WANUNUZI ZAO LA PAMBA WAISHUKURU SERIKALI

Loading...
WANUNUZI wa zao la pamba wameishukuru Serikari kwa kuweka mfumo mzuri wa ununuzi wa zao hilo, ambalo kwa mwaka huu linauzwa kupitia katika minada inayosimamiwa na Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS).

Hata hivyo wanunuzi hao wameiomba Serikali kuziwezesha AMCOS kuwa na maghala makubwa na ya kisasa ya kuhifadhia pamba, lengo likiwa ni kuhakikisha pamba inahifadhiwa kwenye maeneo salama na kuifanya isipoteze ubora.

Kauli hiyo imetolewa jana (Jumanne, Juni 12, 2018) na mmoja wa wanunuzi hao ambaye ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya NGS Investment LTD, Bw. Emmanuel Dandu alipokuwa akizungumzia kuhusu kuanza kwa uchambuaji wa pamba kwa msimu wa mwaka huu.

Alisema awali kabla pamba haijaanza kuuzwa kupitia AMCOS suala la ubora lilikuwa halizingatiwi sana na wakulima kwani  pamba yake ikikataliwa na kampuni moja alikuwa na uhuru wa kuipeleka kwenye kampuni nyingine na, jambo ambalo lilichangia kuisha thamani.

Hata hivyo ameiomba Serikali kuwajengea uwezo viongozi wa Ushirika ili waweze kutekeleza majuku yao kikamilifu na pia isaidie kutoa elimu kwa wanachama juu ya umuhimu na faida za AMCOS ili wakulima wengi waweze kujiunga.

Bw. Dandu ambaye kampuni yao ya NGS Investment LTD, licha ya kujishughulisha na biashara nyingine, pia inamiliki kiwanda cha kuchambua pamba cha Majahida kilichopo wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, ambayo tayari imeshaanza zoezi ya uchambuaji pamba.

Alisema pamba inayochambuliwa katika kiwanda hicho wanainunua kupitia AMCOS walizopangiwa, ambapo alipongeza mfumo huo kwa sababu unawawezesha kupata malighafi kwa urahisi na kwa wakati.

“Wanunuzi wote tunanunua pamba kupitia AMCOS. Serikali imeweka mfumo mzuri unaotuweza wote kununua pamba kadiri ya uwezo wetu. AMCOS zimeagizwa kuuza pamba kwa wanunuzi wote bila ya ubaguzi, tofauti na miaka ya nyuma” alisema.

Akizungumzia kuhusu uwezo wa kiwanda hicho, alisema kina uwezo wa kuchambua tani 40,000 za pamba kwa mwaka, lakini wanalazimika kuchambua wastani wa tani tano  hadi 12 kutokana na changamoto ya upatikanaji wa pamba ya kutosha pamoja na changamoto ya umeme wa uhakika.

Pia aliiomba Serikali iwasaidie wakulima kwa kuwapatia pembejeo kwa wakati pamoja na kuwapa elimu ya mara kwa mara juu ya kulima kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha zao la pamba, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa wakati ili waweze kujiongezea tija.
Na Geofrey Okechi.




Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
WANUNUZI ZAO LA PAMBA WAISHUKURU SERIKALI WANUNUZI ZAO LA PAMBA WAISHUKURU SERIKALI Reviewed by By News Reporter on 6/13/2018 11:24:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.