Loading...

ZANZIBAR KUNUNUA BOTI TANO ZA ABIRIA

Loading...
WIZARA ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, imesema kwa mwaka wa fedha 2018/2019 itanunua meli mpya ya mafuta ambapo mkataba wa ujenzi kati ya serikali na kampuni ya Damen Shipyard ya Uholanzi, umesainiwa Disemba 2017.

Waziri wa wizara hiyo, Sira Ubwa Mamboya, aliyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.

Alisema malipo ya awali yamefanyika ambayo ni sawa na asilimia 30 ya gharama zote za ununuzi wa meli hiyo na matayarisho ya ujenzi wa meli yameanza.

Aidha alisema, kwa mwaka wa fedha 2017/2018, mradi huo ulipangiwa shilingi 18 bilioni kutoka serikalini ambapo hadi Machi 2018, shilingi 11.3 bilioni zimetumika sawa na asilimia 63 za makadirio.

Alisema pia wizara imepanga kununua boti tano ambazo zitatoa huduma katika visiwa vya Tumbatu, Fundo, Kojani, Kisiwapanza na Makoongwe kwa lengo la kuwapatia huduma bora za usafiri wa baharini wananchi.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2017/2018, mradi ulipangiwa kutumia shilingi 18.8 bilioni na hadi kufikia Machi mwaka huu shilingi 11.3 bilioni zimetumika.

Akizungumzia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume, alisema kuna ongezeko la mashirika ya ndege mapya likiwemo shirika la ndege la Fly Pegas kutoka Russia pamoja na ongezeko la safari za ndege za kimataifa.

Alisema katika kipindi hicho Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (ZAA) imehudumia jumla ya safari za ndege 51,669, abiria 1,039,075 katika kiwanja cha ndege cha Unguja na Pemba.

Akizungumzia ujenzi wa jengo jipya la abiria (terminal 3) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Aman Karume, alisema mradi huo unaendelea kumalizia ujenzi wa jengo jipya la abiria, maegesho ya ndege, maegesho ya gari na uwekaji wa vifaa katika uwanja huo.

“Mradi huu unatekelezwa kwa kutumia fedha za mkopo kutoka benki ya Exim ya China pamoja na mchango wa serikali yenyewe,” alisema.

Alisema kwa sasa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa maegesho ya ndege (apron) kwa tabaka la kifusi na kuanza kazi za kumaliza ujenzi wa jengo husika.

Aidha alisema idara ya ujenzi na utunzaji barabara kupitia programu ndogo ya miundombinu na usafirishaji, imepanga kufanya matengenezo kilomita 55.3 za barabara Unguja na Pemba.

Pia alisema idara itaendelea kuzitunza barabara zilizojengwa kwa kuzifanyia usafi na matengenezo ili ziweze kupitika muda wote.

Waziri huyo aliomba kuidhinishiwa shilingi 214.5 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida na maendeleo ya wizara hiyo.

Akiwasilisha hotuba ya kamati ya ardhi na mawasiliano, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleiman Sarhani Said, alisemakamati inaishauri serikali kuharakisha mchakato wa kuifanya idara ya uendeshaji na utunzaji wa barabara (UUB) kuwa wakala wa barabara.
Na Geofrey Okechi.




Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
ZANZIBAR KUNUNUA BOTI TANO ZA ABIRIA ZANZIBAR KUNUNUA BOTI TANO ZA ABIRIA Reviewed by By News Reporter on 6/08/2018 07:39:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.