Loading...

AMUUA MAMA YAKE KWA KUMCHARANGA MAPANGA KISA MALI ZA URITHI

Loading...
MKAZI wa kijiji cha Ilebelebe , Ngassa Mathias (24), anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mama yake mzazi, Nyawamba Dohoi (61), kwa kumcharanga mapanga kichwani hadi kufa.

Tukio hilo limetokea Julai 11, mwaka huu majira ya saa 10 usiku, wakati mama huyo akiwa amelala nyumbani kwake na wajukuu zake wawili.

Imedaiwa kuwa watu wasiojulikana waliingia ndani na kumshambulia mama huyo sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwamo kumkata kichwa kwa mapanga na kufariki dunia.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Simoni Haule, alisema chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali za marehemu alizoachiwa na mumewe na mtoto huyo akidaiwa kutaka kuzimiliki.

“Tunamshikilia mtoto wa marehemu Ngassa Mathias kwa uchunguzi wa awali, inadaiwa ndiye mhusika mkuu wa mauaji ya mama yake mzazi kutokana na kutaka kurithi mali ambazo mama yake aliachiwa na mumewe na upelelezi ukikamilika na kubaini kufanya mauaji atafikishwa mahakamani,” alisema Haule.

“Natoa wito kwa vijana kujishughulisha katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwamo kilimo, na kuacha tabia ya kutaka mali za mirathi na kufikia hatua ya kutoa uhai wa wazazi wao,” aliongeza.

Aidha, Mwenyekiti wa kitongoji cha Kiloleli yalipofanyika mauaji hayo, Solo Bundala, alisema walibaini kufariki kwa mwanamke huyo majira ya saa tatu asubuhi na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.

Alisema kuwa katika kitongoji hicho kumekuwa kukitokea mauaji ya aina hiyo mara kwa mara.
Na Fatma Pembe.




Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
AMUUA MAMA YAKE KWA KUMCHARANGA MAPANGA KISA MALI ZA URITHI AMUUA MAMA YAKE KWA KUMCHARANGA MAPANGA KISA MALI ZA URITHI Reviewed by By News Reporter on 7/14/2018 04:37:00 PM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.