Loading...

NAMNA YA KUISHI NA MPENZI MWENYE MAWAZO HASI

Loading...
MTU mwenye mawazo hasi, ni yule ambaye muda wote anayatazama mambo kwa ubaya, analalamika, analaumu wengine, anapenda kuwashambulia wengine kwa kauli za kuudhi na zisizo za kiungwana na muda wote anaamini kwamba yeye hakosei.

Mtu wa namna hii, mara nyingi huwapa wakati mgumu sana watu wanaomzunguka na mara nyingi hawezi kuwa na marafiki, na hata akiwa nao kila siku atakuwa na kazi ya kuwabadilisha kwa sababu hakuna anayeweza kumvumilia.

Kwa bahati mbaya, wapo watu ambao wameingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na watu wa aina hii. Mnaishi kama wapenzi lakini mwenzako muda wote kazi yake ni kutazama tu makosa yako, kuzungumza mambo mabaya kuhusu wewe, na kukutuhumu kwa mambo mbalimbali, hata ambayo si ya kweli.

Unapokuwa katika uhusiano na mtu wa namna hii, unatakiwa kuwa makini sana kwani inaweza kukuathiri vibaya na mwisho ukaishia kupata maradhi ya moyo, msongo wa mawazo, kudhoofika mwili na kuona kama dunia yote imepoteza kabisa maana.

Ukiwa na mpenzi wa aina hii, utajihisi muda wote huna furaha, muda wote unatamani kama uachane naye au ujitenge naye mahali ambapo hamtaonana mara kwa mara na kadhalika lakini kwa bahati mbaya, wengi hushindwa kuchukua hatua yoyote na kuendelea kuwa mateka wa mapenzi.

Jambo la kwanza, unatakiwa kulitambua tatizo lililopo. Kwamba pengine mpenzi wako ni mtu mwenye tabia hizo nilizozitaja na hukuwahi kujua kama anasumbuliwa na tatizo gani, pengine ulikuwa unaamini kwamba wewe ndiyo mwenye matatizo, anza leo kumchunguza kwa makini ili uwe na majibu sahihi.

Wapo watu ambao wamezaliwa hivyo, au ugumu wa maisha na changamoto mbalimbali walizokutana nazo zimewafanya wawe ‘negative’, na kawaida mtu wa namna hii, anakuwa na hisia na mawazo hasi kwa kila mtu anayemmudu.

Anaweza kujibizana hovyo na mkewe au mumewe, majirani, ndugu zake wa karibu au hata watu ambao hawafahamiani. Yaani kwa lugha nyepesi, anakuwa na tabia inayofanana hata anapokuwa na watu tofauti, yeye muda wote.

Baada ya kugundua kwamba kumbe hakufanyii wewe tu vituko vya aina hiyo, unatakiwa kuelewa kwamba ana matatizo na ana hitaji msaada. Ni kama mgonjwa wa Malaria, huwezi kumchukia kwa sababu anaumwa bali utamsaidia ili apone.

Kuwa na hisia hasi muda wote ni tatizo kubwa, ni maradhi ya akili na hisia! Mtu mwenye hisia au mawazo hasi muda wote, ukiachilia ukweli kwamba anaweza kuwasababishia madhara ya kihisia watu wanaomzunguka, yeye hupata madhara zaidi ndani kwa ndani.  Mtu wa namna hii anaweza kuanza kuumwa na mkimpeleka hospitali, vipimo vyote vikaonesha kwamba haumwi chochote, kumbe chanzo ni zile hisia zake hasi na mawazo ‘negative’.

Katika hatua za kumsaidia, unatakiwa uanze kwa kumfanya yeye pia agundue kwamba ana tatizo na hayupo sawa kwa sababu watu wa aina hii huwa wanaamini kwamba wao hawakosei, wanaamini wewe ndiye mwenye matatizo na wala siyo wao. Ukiona huna ujasiri wa kumfanya agundue tatizo lake, unaweza kuwashirikisha wataalamu wa saikolojia.

Hatua nyingine ni kujitahidi kuyakwepa mawazo hasi yake. Unaweza kuwa umevaa vizuri na kupendeza na wewe unaamini umependeza lakini yeye akakutolea maneno yanayokufanya ujione kama hujavaa nguo, usiyaamini aliyoyasema bali jiambie ndani ya moyo kwamba anaumwa ndiyo maana anazungumza hivyo.

Katika kila baya analokufanyia, wewe tazama upande wa pili kwa kugeuza baya hilo kuwa zuri. Muoneshe kwamba hata kama yeye anakutoa kasoro na kukukosoa unajiamini na upo imara.
Na Neema Joshua.



Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
NAMNA YA KUISHI NA MPENZI MWENYE MAWAZO HASI NAMNA YA KUISHI NA MPENZI MWENYE MAWAZO HASI Reviewed by By News Reporter on 7/13/2018 10:12:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.