Loading...
Emmerson Mnangagwa ameapishwa kushika hatamu za uongozi wa Zimbabwe kwa miaka mitano ijayo, karibu mwezi mmoja baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Mahakama ya katiba Ijumaa wiki hii ilithibitisha ushindi wa asilimia 50 aliopata Mnangagwa katika uchaguzi wa Julai 30, ikitupilia mbali shauri lililofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa upinzani Nelson Chamisa.
Mamia kwa maelfu ya watu walimiminika katika Uwanja wa Taifa Mjini Harare, kushuhudia kuapishwa kwa Mnangagwa ambaye alichukua madaraka Novemba mwaka jana, baada ya Jeshi kuingilia kati na kumuondoa kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe.
"Mimi Emmerson Dambudzo Mnangagwa naapa kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Zimbabwe, na nitaiheshimu, kuitetea na kuilinda katiba ya Zimbabwe,"alisema kiongozi huyo katika kiapo kilichoongozwa na Jaji Mkuu Luke Malaba.
Kiongozi huyo ameahidi kulinda na kutetea haki za raia wa Zimbabwe.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Afrika akiwemo, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Hata hivyo Mnangagwa anakabiliwa na kazi nzito ya kurejesha umoja katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Na Fatma Pembe.
Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
MNANGAGWA AAPISHWA, AAHIDI KULINDA HAKI ZA RAIA WA ZIMBABWE
Reviewed by By News Reporter
on
8/27/2018 06:20:00 AM
Rating:
Hakuna maoni: