Loading...

HATIMAYE DOS SANTOS WA ANGOLA ANG'ATUKA RASMI KWENYE SIASA, BAADA YA KUKAA MADARAKANI KWA MIAKA 38

Loading...
Rais Joao Lourenco wa Angola amechaguliwa rasmi kuwa kiongozi wa chama tawala, MPLA, akichukuwa mikoba ya rais wa zamani, Jose Eduardo dos Santos aliyekuwa akizitawala siasa za nchi hiyo kwa takribani miongo minne.

Akiwa amehudumu kwenye nafasi ya urais tangu Agosti 2017, Lourenco alipata asilimia 98.59 ya kura za wajumbe 2,951 wa chama hicho tawala siku ya Jumamosi (Septemba 8), na hivyo kukamilishiwa hatua za kumilikishwa mamlaka ya juu kabisa kwenye taasisi zote muhimu za nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

"Kwa nguvu za jana na za leo tunajenga kesho yetu, tunaweza kusahihisha kilichokosewa," Lourenco aliwaambia wajumbe wa mkutano mkuu wa sita usiokuwa wa kawaida wa MPLA.

Tangu aingie madarakani, Lourenco amekuwa akionesha kutafautiana kisera na kimkakati na mtangulizi wake, dos Santos, huku akielezea bayana kuwa anataka kuzizika kabisa siasa za zamani.
"Ndugu zangu, sote tunajuwa kuwa tutaweza tu kuujenga mustakabali mwema kama tunao uthubutu wa kweli wa kurekebisha kisicho sahihi - ufisadi na udugunaizesheni, uzembe na kukiuka sheria - mambo ambayo yamekuwa yakitokea katika miaka ya hivi karibuni," alisema Lourenco.

Hatimaye dos Santos ang'atuka rasmi

Hata hivyo, dos Santos aliwaaga wajumbe wa mkutano huo mkuu wa MPLA kwa kuwaambia kuwa hajutii alichokifanya kwenye utawala wake. "Leo naondoka nikiwa kifua mbele na nakabidhisha kijiti kwa Komredi Joao Lourenco," alisema dos Santos kwenye makao makuu ya chama tawala mjini Luanda. 

Mpiganaji huyo wa ukombozi mwenye umri wa miaka 76 hakuwania tena urais kwenye uchaguzi wa Agosti 2017 na alimkabidhi madaraka waziri wake wa ulinzi, Lourenco, mwenye umri wa miaka 64. Hata hivyo, aliendelea kushikilia nafasi ya juu kabisa kwenye chama, ambako ndiko hasa nguvu za utawala wa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ziliko.

Lakini siku ya Jumamosi, "Komredi Nambari Moja" - kama alivyokuwa akiitwa - hatimaye aliwachia udhibiti wa MPLA kwa Lourenco, huku akikiri baadhi ya makosa wakati wa utawala wake. "Hakuna binaadamu asiye makosa, nami nakisia kuwa nilifanya makosa pia," alisema dos Santos.
Na Paskali Joseph.



Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
HATIMAYE DOS SANTOS WA ANGOLA ANG'ATUKA RASMI KWENYE SIASA, BAADA YA KUKAA MADARAKANI KWA MIAKA 38 HATIMAYE DOS SANTOS WA ANGOLA ANG'ATUKA RASMI KWENYE SIASA, BAADA YA KUKAA MADARAKANI KWA MIAKA 38 Reviewed by By News Reporter on 9/09/2018 11:36:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.