Loading...
Tanzania ni mojawapo ya nchi zilizobarikiwa kuwa na maliasili zenye kuvutia kwa kila hali.
Tukianza na kuangazia maajabu ya ziwa Ngosi lililopo mkoani Mbeya, wilaya ya Rungwe katika milima ya Uporoto.
Inasemekana ziwa hili ni ziwa kreta na la pili kwa ukubwa duniani baada ya ziwa kama hilo lililopo nchini Ethiopia.
Moja ya maajabu ya ziwa Ngosi ni kwamba lina muonekano wa ramani ya Afrika. Pili, ni ziwa lililopo juu milimani. Lina kina cha mita 74.
Pamoja na sifa nyingi na maajabu yake bado halijawa sehemu ya kivutio kikubwa cha utalii nchini.
Licha ya kuwepo kwa ziwa Ngosi, nimeona ni vema nikalielezea kwa kifupi ziwa jingine lisilofahamika sana lakini baadhi ya sifa zake zinafanana na ziwa Ngosi.
Ziwa hilo linajulikana kama ziwa Challa au Lake Challa kama watu walivyozowea kuliita. Lake Challa linapatikana mkoani Kilimanjaro, wilaya ya Rombo na lipo mpakani kati ya Tanzania na Kenya. Ziwa hili nalo ni kreta lenye kina cha mita 78.
Ziwa Challa lina historia ya kusisimua ambapo linapata maji kupitia mto uliopo chini ya miamba na inasemeka maji hayo yanatoka mlima Kilimanjaro. Ziwa hili kama ilivyo kwa ziwa Ngosi bado halijulikani sana ingawa kwa miaka ya hivi karibuni watalii wameanza kutembelea. Yapo mengi yaliyomo kwenye ziwa hili.
Katika maziwa yote mawili maji yake hubadilika rangi kutegemeana na wakati kwani maziwa haya yamezungukwa na miti. Kingo za maziwa haya zina mteremko mkali. Kwa upande wa ziwa Challa kuna njia maaluum inayoteremkia ziwani hasa kwa wale wanaopenda kwenda kuliona ziwa hilo. Ziwa Challa pia linaweza kuonekana vizuri ukiwa kwenye mdule uliojengwa jirani na ziwa hilo unaomilikiwa na mwekezaji aliyewekeza kwa kujenga "lodge" katika eneo hilo.
Rai yangu ni kwamba idara zinazohusika na utangazaji wa utalii zifanye jitihada za makusudi za kutangaza vivutio tulivyonavyo kwa lengo la kuliingizia taifa mapato.
Nasi wengine tupatapo wasaa tutembelee vivutio vilivyopo maeneo mbalimbali kwani kuna mengi ya kujifunza.
Na Geofrey Okechi.
Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com au sms-whatsapp: +255765112259
KUELEKEA TAMASHA LA URIDHI WETU, TUONE MAAJABU YA ZIWA NGOSI NA CHALLA
Reviewed by By News Reporter
on
9/15/2018 07:09:00 AM
Rating:
Hakuna maoni: