Loading...

VYUO VINGINE VYAFUTIWA USAJILI NA NACTE

Loading...
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), limevifutia usajili vyuo vitatu na kuvizuia vingine vinne kudahili wanafunzi mpaka dosari zilizoonekana zitakapopatiwa ufumbuzi.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti Ubora wa Nacte, Dk. Jofrey Oleke.

Alivitaja vyuo vilivyofutiwa usajili kuwa ni Cageti College of Health Sciences, Mafinga College of Bussines Education vilivyopo Mafinga na Mbozi School of Nursing kilichopo Mbozi.

Dk. Oleke alitaja vyuo vinne vilivyozuiliwa kudahili wanafunzi wapya ni KAPS Community Development Institute, School of Dental Therapists na Tukuyu School of Nursing vyote vilivyopo Mbeya.

Alisema chuo kingine ambacho kimezuiliwa kudahili ni Institute of Procurement and Supply kilichoko Dar es Salaam.

Dk. Oleke alisema dosari hizo zimebainika kupitia ukaguzi wa vyuo uliofanyika kwa miezi mitatu kuanzia Juni kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo jumla ya vyuo 59 vilikaguliwa.

Alisema katika ukaguzi huo vyuo 52 vilionekana kukidhi vigezo vya kutoa mafunzo na vyuo hivyo saba vilikutwa na mapungufu makubwa.

Alisema uamuzi wa kuvifutia vyuo hivyo usajili ulizingatia kifungu cha 20 (1) cha Kanuni za Usajili wa Vyuo vya Ufundi, mwaka 2001.

Alisema Baraza limeviandikia barua vyuo hivyo kwa kuvitaka kuhakikisha wanafunzi walioko kwenye programu walizokuwa wanazitoa wanahamishiwa vyuo vingine vilivyosajiliwa na Nacte kutoa programu hiyo.

Alisema vyuo vinne vilivyositishiwa kudahili wanafunzi wapya kuanzia mwaka wa masomo 2018/19 vimeruhusiwa kuendelea na masomo kwa wanafunzi waliopo kama kawaida mpaka watakapohitimu mafunzo yao.

Mkurugenzi huyo alibainisha kasoro kubwa ambayo mara kwa mara wakifanya ukaguzi hubainika ni ukosefu au upungufu wa walimu na miundombinu isiyokidhi.
Na Fadhili Daudi.



Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com.
VYUO VINGINE VYAFUTIWA USAJILI NA NACTE VYUO VINGINE VYAFUTIWA USAJILI NA NACTE Reviewed by By News Reporter on 10/11/2018 07:41:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.