Loading...

HOFU YA KIMBUNGA YAZUKA TANZANIA NA NCHI JIRANI

Loading...
Kumezuka hofu ya kimbunga kwenye upwa wa magharibi wa Bahari ya Hindi hususan katika nchi za Msumbiji, Tanzania, visiwa vya Komoro na Madagaska.

Mtandao uliobobea kwenye masuala ya hali ya hewa wa AccuWeather wa nchini Marekani umeripoti kuwa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa katika bahari ya Hindi huenda ukapelekea kutokea Kimbunga kitakachopewa jina la Kenneth.

Iwapo kimbunga hicho kitatokea, kinatazamiwa kuathiri maeneo ya kuanzia Lindi kusini mwa Tanzania mpaka Pemba kaskazini mwa Msumbiji, Komoro na Madagaska.

Mtandao huo pia umebainisha kuwa mgandamizo huo wa baharini unaweza kupoteza makali na kimbunga kisitokee, ila badala yake mvua kubwa zinaweza kutokea na kuathiri maeneo hayo.

"Mvua kali zinazoweza kusababisha mafuriko na mmomonyoko wa udongo katika maeneo kama Masasi na Tunduru nchini Tanzania, pia Marrupu na Montepuez kwa upande wa Msumbiji," imeeleza taarifa ta AccuWeather.

TMA YATOA TAHADHARI

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetoa taarifa kwa umma Jumatatu Aprili 22, kuhusiana na hali hiyo kwenye bahari ya Hindi, na kusema mifumo ya hali ya hewa inaonesha mgandamizo mdogo wa hewa katika eneo la kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.

"Mgandamizo huo haujafikia kiwango cha kimbunga kamili na upo mbali na pwani ya nchi yetu kwa sasa. Inatarajiwa mgandamizo huo utaimarika zaidi katika kipindi kifupi na kutawala mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa nchini mwetu," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mamlaka hiyo pia imetoa utabiri wa hali ya hewa kwa siku tano kati ya Aprili 22 mpaka Aprili 26.

Utabiri huo unatoa tahadhari kuwa siku ya Ijumaa, Aprili 26 kunategemewa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa baharini katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara.

"Tafadhali chukua hatua, uwezekano wa kutoke ni mkubwa na kiwango cha athari zinazoweza kutokea ni mkubwa," taarifa hiyo ya (TMA).

Kwa mujibu wa Meneja wa Utabiri wa Hali ya Hewa wa Kimataifa wa AccuWeather, kimbunga Kenneth kinatarajiwa kuzikumba Tanzania na Msumbiji Alhamisi usiku ama mapema Ijumaa wiki hii.
Na Yohana Petro.
.
.
Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com.
HOFU YA KIMBUNGA YAZUKA TANZANIA NA NCHI JIRANI HOFU YA KIMBUNGA YAZUKA TANZANIA NA NCHI JIRANI Reviewed by By News Reporter on 4/24/2019 08:11:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.