Loading...

VIFAA KWA AJILI YA UPIMAJI HOMA YA DENGUE VYASAMBAZWA DAR

Loading...
MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Yudas Ndugile, amesema wameshasambaza vitendanishi vya maabara kwa ajili ya ugonjwa wa homa ya dengue katika hospitali zote za Serikali jijini humo.

Jiji la Dar es Salaam lina wagonjwa zaidi ya 1,200 ambao wameshabainika kuwa na homa hiyo ya dengue, hivyo vifaa hivyo vitasaidia kupunguza gharama za upimaji kutoka Sh. 65,000 hadi Sh. 15,000.

Akizungumza na gazeti la Nipashe, Dk Ndugile, alisema kuwapo kwa vipimo hivyo kumerahisisha huduma ya upimaji wa homa hiyo kutokana na awali wananchi walikuwa wakitumia fedha nyingi katika hospitali binafsi.

“Tayari katika hospitali zote za Serikali za mkoa huu tumeshasambaza vitendanishi vya maabara kwa ajili ya kupima homa ya dengue. Sasa wagonjwa watapata huduma bila ya usumbufu kwa gharama nafuu kabisa,” alisema Dk. Ndugile.

Alisema vipimo hivyo vinapatikana katika hospitali za Mwananyamala, Ilala, Temeke, vijibweni na Mnazi Mmoja.

Kuhusu wagonjwa waliopo katika hospitali za binafsi, Dk. Ndugile alisema, wanaweza kupata huduma ya vipimo kwa bei nafuu endapo wataenda kutibiwa katika hospitali za Serikali.

Homa ya dengue ni ugonjwa wa kitropiki unaosababishwa na virusi maarufu kama dengue.

Dalili za ugonjwa huu huanza siku tatu hadi kumi na nne baada ya kuambukizwa.

Baadhi ya dalili ni homa kali, kuumwa na kichwa, kuota vipele kwenye ngozi na maumivu kwenye misuli na maungio.

Dalili kubwa ni ile ya kuvuja damu, ambayo huifanya mishipa ya damu inayobeba damu kupasuka.

Kwa kawaida matibabu huchukua siku tatu hadi saba hadi mgonjwa kupona na hakuna dawa ya chanjo inayofanya kazi kuwakinga watu dhidi ya virusi vya dengue.
Na Saidi Mchuka.
.
.
Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com.
VIFAA KWA AJILI YA UPIMAJI HOMA YA DENGUE VYASAMBAZWA DAR VIFAA KWA AJILI YA UPIMAJI HOMA YA DENGUE VYASAMBAZWA DAR Reviewed by By News Reporter on 5/15/2019 09:14:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.