Loading...

MAPYA YAIBUKA MAUAJI KANISANI

Loading...
JESHI la Polisi Mkoa wa Singida limedai zaidi ya risasi 10 zilitumika katika tukio la mauaji dhidi ya Isack Petro (28), aliyeuawa kwa kupigwa risasi kisogoni ndani ya Kanisa la Waadventista Wasabato lililoko Kijiji cha Kazikazi, Kata ya Kitaraka, Itigi mkoani Singida.

Tukio hilo lilitokea Jumamosi ndani ya kanisa hilo wakati  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Itigi, Pius Luhende (54), na watu wengine sita wakidaiwa kushiriki mauaji hayo kwa kupiga zaidi ya risasi 10 ndani ya kanisa. Watuhumiwa hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Singida.

Mbali na Mkurugenzi huyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike, akizungumza na waandishi wa habari jana, aliwataja watuhumiwa ambao wanawashikilia kuwa ni pamoja na askari wawili wa wanyamapori, Rodey Elias (42), Makoye Steven, Ofisa Kilimo, Sylvan Lugwisha (50), Ofisa Sheria, Erick Paul (31), Ofisa Tarafa Itigi, Eliuta Agustino (43) na Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Yusuf John (25).

Akieleza kuhusu tukio hilo, Kamanda Njewike alidai kuwa lilitokea Jumamosi majira ya saa nane mchana, Mkurugenzi Luhende, akiwa na timu ya watu sita, walipokwenda kanisani huko kwa lengo la kuwakamata watuhumiwa.

Alidai kuwa Mkurugenzi Luhende na wenzake walikuwa wanawatafuta watuhumiwa wanaodaiwa kufanya kosa la kuharibu mali katika shamba la Tanganyika Parkers.
Kamanda Njewike alidai kuwa shamba hilo linamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Itigi ambako Isack (marehemu) alikuwa anaishi.

Alidai kuwa siku ya tukio, mkurugenzi na wote wanaoshikiliwa, waliamua kuingia mtaani kuwasaka watuhumiwa hao baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Rose Andrew, aliyedai kuharibiwa mali yake shambani humo.

“Wakati wanaendelea kuwasaka, ndipo wakagundua baadhi yao wapo ibadani kwenye kanisa hilo la Wasabato," Kamanda Njewike alidai.

Aliongeza: "Baada ya kufika kwenye kanisa, Mkurugenzi Luhende aliingia ibadani akitaka kuwakamata hao waliokuwa wanadaiwa kuwa ni watuhumiwa wa uharibifu wa mali shambani. Hali hiyo ilisababisha kutokea kwa vurugu kanisani."
Alidai kuwa, wakati vurugu hiyo ikiendelea, mkurugenzi huyo alitoka nje na kufunga mlango wa kuingia kanisani, ndipo askari wanyamapori walioongozana naye wakaanza kufyatua risasi kanisani humo.

“Moja ya risasi zilizofyatuliwa ilimpiga Isack eneo la kisogoni na kufariki dunia hapohapo. Risasi zilizopigwa ni zaidi ya 10 na uchunguzi wa tukio hili unaendelea wakati watuhumiwa wote saba wakiwa mahabusu."

Kamanda Njewike alisema watahakikisha watuhumiwa wanafikishwa mahakamani mapema kujibu tuhuma zinazowakabili.

Taarifa kutoka eneo la tukio zilizoifikia Nipashe, zilidai kuwa mmoja wa watuhumiwa hao saba, baada ya kutokea vurugu kanisani, alirudi kwenye gari na kuchukua silaha.

Hata hivyo, Kamanda Njewike, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema hana uhakika nalo.

Nipashe pia ilitaka kujua kutoka kwa kamanda huyo kama watuhumiwa wanayo mamlaka ya kuendesha msako wa aina hiyo na akasema: "Mwenyekiti wa serikali ya mtaa ana mamlaka ya kukamata, lakini kwa tukio lililotokea na nguvu iliyotumika, tunachunguza kama mamlaka hiyo ndivyo inavyomwelekeza Mkurugenzi."

Source: NIPASHE.



Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com.
MAPYA YAIBUKA MAUAJI KANISANI MAPYA YAIBUKA MAUAJI KANISANI Reviewed by By News Reporter on 2/06/2019 11:10:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.