Loading...

SABABU 3 MAUAJI YA WATOTO MKOANI NJOMBE

Loading...
TIMU ya Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema imebaini sababu tatu zilizochangia kuwapo kwa mauaji ya watoto mkoani Njombe.

Pia timu hiyo imeutaka uongozi wa Mkoa wa Njombe kuhakikisha ajenda ya ulinzi na usalama wa mtoto inakuwa ya kudumu mkoani humo.

Kiongozi wa timu hiyo, Hanisa Selengu, akizungumza mjini Njombe jana, alizitaja sababu zilizochangia kuwapo kwa mauaji dhidi ya watoto kuwa ni tabia ya kukumbatia mila potofu na zisizofaa zinazochangia kuwa na mifarakano katika jamii.

Alisema sababu zingine ambazo timu yake imebaini ni migogoro ya kifamilia ambayo imekuwa ikisababishwa na visasi vya wazazi na ndugu pamoja na desturi ya ukimya na ugumu wa kueleza uhalifu unaotokea.

Selengu alisema katika siku 10 walizokaa mkoani humo, timu yake imejifunza masuala mbalimbali kutoka kwa jamii na kubaini mauaji hayo yanafanyika kutokana na changamoto hizo tatu.

Alisema ajenda ya ulinzi wa mtoto isifanyike tu panapotokea matukio ya utekaji na mauaji ya watoto, bali iendelee kupewa mkazo na kusisitizwa na viongozi mkoani humo.

Aliutaka uongozi wa Mkoa wa Njombe kuifanya ajenda hiyo kuwa ya kudumu na kupewa nguvu na viongozi katika mikutano mbalimbali wanayofanya na wananchi.

Aliongeza kuwa, ili kuhakikisha ulinzi na usalama kwa mtoto, Kamati za Ulinzi na Usalama wa wanawake na watoto zina jukumu kubwa la kuhakikisha mtoto anakuwa salama na kuhakikisha agenda ya  usalama kwa watoto inapewa kipaumbele zaidi ili kumhakikishia mtoto huyo ulinzi na usalama.

Alisema timu yake inapendekeza mkoa kuhakikisha mipango ya kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zinatengewa bajeti na kutekeleza majukumu yake.

"Huduma za kisaikolojia na kijamii ziendelee kutolewa kwa familia zilizopoteza watoto na makundi maalum," alisema kiongozi huyo na kubainisha kuwa mapendekezo mengine ya timu yake kuwa ni kuendelea kuelimisha na kuhimiza mazingira salama kwa watoto nyumbani, shuleni na mazingira yanayowazunguka.

Selengu pia alisema kuna haja kuendelea kufanya mikutano ya mara kwa mara kwa familia, makundi maalum na wanajamii kuhusu mila na desturi potofu.

Mwezi uliopita, kuliripotiwa matukio ya utekaji na mauaji dhidi ya watoto mkoani Njombe, huku wanaotekeleza ukatili huo wakidaiwa kunyofoa baadhi ya viungo kwenye miili ya watoto wanaowaua.

Tayari watu watatu wamefikishwa mahakamani na kushtakiwa huku wengine 27 wakiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na matukio hayo.
Na Mary Mkeu.



Una maoni? Una habari ambayo ungependa tuichapishe? Tuma ujumbe kwa mhariri mkuu:dundiikaonline@gmail.com.
SABABU 3 MAUAJI YA WATOTO MKOANI NJOMBE SABABU 3 MAUAJI YA WATOTO MKOANI NJOMBE Reviewed by By News Reporter on 2/15/2019 07:08:00 AM Rating: 5

Hakuna maoni:

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.